Pasta Ng'ang'a awataka waumini kumuombea baada ya bili ya umeme kupanda hadi 40k

“Ombeeni huyu mtoto wa kiume, hana nafasi, kwa Kenya Power wameongeza mara mbili hiyo bei," alisema.

Muhtasari

• Ng’ang’a hata hivyo alisema kwamba hakubaliani na nyongeza hiyo ambayo hajui imetokana na nini kwani kwake hana disco.

Mchungaji Ng'ang'a atoa neno kwa wanaokosoa matamshi yake.
Mchungaji Ng'ang'a atoa neno kwa wanaokosoa matamshi yake.
Image: Screengrab//Sasa TV

Mchungaji mwenye utata kutoka kanisa la Neno Evangelism, James Maina Ng’ang’a amewataka waumini wa kanisa lake kumkumbuka katika maombi baada ya kudai kuwa shirika la umeme nchini, KPLC limemuongezea bili ya umeme mara dufu.

Ng’ang’a alikuwa anahubiri katika moja ya mahubiri yake ambapo aligusia suala la maisha magumu na kukumbuka kwamba hata kwake hali imebadilika ghafla bili yake ya umeme ikiongezeka kutoka shilingi elfu 20 za kawaida hadi shilingi elfu 40.

Ng’ang’a hata hivyo alisema kwamba hakubaliani na nyongeza hiyo ambayo hajui imetokana na nini kwani kwake hana disco ambayo kwamba ingekuwa ndio inatumia umeme wa kiasi hicho cha pesa.

“Ombeeni huyu mtoto wa kiume, hana nafasi, kwa Kenya Power wameongeza mara mbili hiyo bei, kwangu nimeona nimewekewa 40k, yote hiyo nyumba tu na sina disco ndani kwani nimetumia na nini? Kutoka 20k hadi 40k, wakora hawa!” Ng’ang’a alisema.

Aidha alizidi kutilia shaka bili hiyo akisema kwamba si ya kweli hata kidogo.

“40k bili ya nyumba tu? Na ukiona mimi nimewekewa hivyo na wewe?” aliuliza.

Ng’ang’a alitumia nafasi hiyo kuwataka waumini kuwaombea watoto wote wa kiume akisema kwamba hali ya maisha imekuwa juu na pia wanawake wao wanazidi kuwasukuma hadi mwisho wa reli wakitaka vitu vyenye gharama.

“Sasa huyu boychild stima ndio hiyo, ndio nimesikia imebadilika na hamtaki mnataka human hair ati ile ya kutoka sijui wapi… watu wenigne hawataki nywele zao za kawaida, shida ni nini? Mtoto wa kiume mfuta ni yeye, unga umepanda bei ni yeye, nguo zinavaliwa ni yeye…” Ng’ang’a alisema.