Vanessa Mdee avunja kimya baada ya Mkenya Shorn Arwa kumtaka kurudi katika muziki

"Najua Vanessa amechukua mapumziko na hafanyi muziki lakini tafadhali, tamasha la mwisho basi Vanessa,” alisema Shorn Arwa.

Muhtasari

• Mrembo huyo anayeishi Uingereza alisema kwamba kinachomfanya kutaka Mdee kurudi ni kwa sababu siku hizi wasanii wa kike wengi hawana maudhui ya kuwaimbia mashabiki wao Zaidi ya kelele tu.

Shorn Arwa na Vanessa Mdee.
Shorn Arwa na Vanessa Mdee.
Image: Instagram

Msanii wa muda mrefu wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee hatimaye ametoa tamko lake baada ya mwanablogu wa Kenya, Shorn Arwa kumtaka kurudisha fikira nyuma na kurejelea uimbaji tena.

Itakumbukwa Vanessa Mdee amekuwa nje ya ulingo wa Sanaa kwa takribani miaka minne sasa baada ya kuingia katika ndoa na msanii wa Marekani, Rotimi.

Vanessa Mdee hivi majuzi akimsherehekea Rotimi siku yake ya kuzaliwa, alidokeza kwamba hana fikira au wazo lolote la kurudi katika muziki hivi karibuni, akisema kwamba kwa sasa anazingatia Zaidi kuwapa wanawe wawili malezi na uwepo wa mama muda wote.

Shorn Arwa alimbembeleza Mdee na kumtaja kuwa malkia wa muziki wa Afrika Mashariki ambaye hajapata wa kuliziba pengo lake baada ya kuhamia Marekani kuungana na Rotimi.

“Rudisheni Vanessa Mdee kwenye muziki, huyu mrembo alikuwa ni wa moto sana kimuziki, ninaweza sema kwamba katika ukanda wa Afrika Mashariki, hakuna msanii wa kike anayeweza kumfunika Vanessa Mdee,” Arwa alisema katika moja ya video aliyopakia kwenye Instagram yake.

Mrembo huyo anayeishi Uingereza alisema kwamba kinachomfanya kutaka Mdee kurudi ni kwa sababu siku hizi wasanii wa kike wengi hawana maudhui ya kuwaimbia mashabiki wao Zaidi ya kelele tu.

“Siku hizi wasanii wanashinda wakiimba tu ooh makalio ni makubwa ooh… hapana! Tunataka Vanessa Mdee arudi, tunataka miziki inayozungumza na nafsi zetu, najua Vanessa amechukua mapumziko na hafanyi muziki lakini tafadhali, tamasha la mwisho basi Vanessa,” alisema.

Baada ya ombi hilo, Vanessa Mdee alifika kwenye video hiyo na kumjibu Arwa akisema kwamba amelisikia ombi lake na atalifanyia kazi hivi karibuni.

“Nimekusikiliza dadangu,” Vanessa alijibu.