Sababu ya Babu Owino kuchukua breki katika masomo yake ya shahada ya 3 ya uzamili

Mbunge huyo msomi ametajwa kuwa huenda atajitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana Nairobi uchaguzi mkuu wa 2027.

Muhtasari

• “Ninapiga kurasa hizi kwa nguvu katika mpango wangu wa kuhakikisha siwaonei huruma watahini wangu,” Owino alisema.

BABU OWINO.
BABU OWINO.
Image: FACEBOOK//BABU OWINO

Mbunge wa Embakasi Msshariki Babu Owino amefichua kwamba katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, amekuwa akijishughulisha na kubukua vitabu akifanya maandalizi kwa ajili ya mtihani wake wa kufuzu shahada ya tatu ya uzamili.

Mbunge huyo sasa amesema kwamba atachukua mapumziko ya muda kukaa mbali na vitabu kwa muda kwa ajili ya kujipa muda ili kushiriki katika mchakato wa chama chake cha ODM wa kuandikisha wanachama Zaidi jijini Nairobi.

“Kwa muda wa mwezi mmoja uliopita, nimekuwa nikila vitabu kama viazi vikuu nikijiandaa kwa mitihani yangu ya Shahada ya 3 ya Uzamili. Lakini nitapumzika kwa muda mfupi kwa shughuli ya kuajiri ODM jijini Nairobi kabla ya kuanza tena mashambulizi yangu ya kitaaluma. Mungu anibariki,” Babu alisema.

 Mbunge huyo msomi ambaye ametajwa kuwa huenda atajitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana Nairobi uchaguzi mkuu wa 2027 alizidi kujitapa akisema kwamba kwa kawaida yeye huwa haonei vitabu huruma pindi anapoketi kuvibukua.

“Ninapiga kurasa hizi kwa nguvu katika mpango wangu wa kuhakikisha siwaonei huruma watahini wangu,” Owino alisema.

Katika chapisho hilo, Owino alikuwa ameketi mezani na mbele yako kukiwa na rundo la vitabu ainati.