Bahati afichua kwa nini yeye na mkewe Diana hawajapata nafasi ya kulala kwa saa 28

Bahati alipakia picha wakiwa na Diana ndani ya gari lao la kifahari na wote walionekana wenye uchovu na macho yaliyozingirwa na ukungu mwingi kutokana na usingizi mzito.

Muhtasari

• Hata hivyo, hawakutoa maelezo Zaidi kuhusu mradi huo ambao wameuandaa kwa ajili ya mwaka huu ambao tayari robo yake ya kwanza inaelekea kukatika .

Bahati na mkewe Diana
Bahati na mkewe Diana
Image: Instagram

Msanii Kevin Kioko maarufu kama Bahati amewafichua mashabiki wake kwamba katika kipindi cha saa 28 zilizopita, yeye na mke wake Diana Marua hawajapata nafasi ya kutuliza vichwa vyao japo kwa lepe la usingizi.

Bahati alipakia picha wakiwa na Diana ndani ya gari lao la kifahari na wote walionekana wenye uchovu na macho yaliyozingirwa na ukungu mwingi kutokana na usingizi mzito.

Msanii huyo wa ‘Abebo’ alifichua kwamba hawajachagua kutolala kwa kipindi hicho chote cha siku nzima na saa kadhaa juu bali ni kutokana na shughuli nyingi ambazo wamejikita kufanya kwa ajili ya mashabiki wao.

Kijana huyo kutoka Mathare ambaye pia alijaribu guu lake la bahati katika uchaguzi mkuu uliopita kama mbunge wa eneo hilo lakini akafeli alisema kwamba kuna mradi mkubwa sana ambao yeye na Diana wanaendelea kuusuka – mradi ambao kwa maneno na fikira zake utakuwa mkubwa Zaidi kwa mwaka 2024.

“Hatujalala kwa Saa 28 zilizopita... Tumekuandalia Project Kubwa kwa ajili yako mwaka huu wa 2024... Mrembo amechoka wacha nimpeleke Nyumbani akalale,” Bahati alisema.

Hata hivyo, hawakutoa maelezo Zaidi kuhusu mradi huo ambao wameuandaa kwa ajili ya mwaka huu ambao tayari robo yake ya kwanza inaelekea kukatika .

Bahati tangu apoteze katika uchaguzi wa ubunge Mathare Agosti 2022, hajakuwa akionekana sana katika kuachia miziki bali amekuwa Zaidi katika kusukuma chapa ya Diana Marua kuzidi kupata nguvu.

Miezi michache iliyopita, Diana alifikisha wafuasi Zaidi ya milioni moja kwenye YouTube na kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Kenya kufikisha idadi hiyo kubwa ya ufuasi katika mtandao huo wa video.