Embarambamba ni chaguo stahiki kwa Wakenya sababu hamthamini maudhui safi - Ezekiel Mutua

Wakenya walimtaka Mutua kumkomesha Embarambamba i baada ya msanii huyo kutoka Kisii kuachia kionjo cha wimbo wake ‘Tuko uchi’ akionekana kucheza densi bila nguo, Zaidi ya taulo pekee.

Muhtasari

• "Hata hivyo, ninaamini kuwa Kenya inastahili Embarambara. Hatuthamini maudhui safi,” Mutua alisema kupitia Facebook.

Embarambamba.
Embarambamba.
Image: Screengrab

Mkurugenzi mkuu wa halimashauri ya kusimamia hakimiliki za kazi za kisanaa nchini MCSK, Ezekiel Mutua amesema kwamba msanii wa injili mwenye vitimbi, Chris Embarambamba ni picha halisi ya kile ambacho Wakenya wengi wanashabiki.

Mutua ambaye aliwahi kuwa mkurugenzi katika bodi ya kutathmini ubora wa kazi za Sanaa, KFCB alisema kwamba amepata watu wengi wakimtaka kuingilia kati kumkomesha Embarambamba ambaye amekuwa akiachia nyimbo zenye maudhui chafu akijificha nyumba ya injili.

Hata hivyo, Mutua akiwajibu, alisema kwamba kwa vile Wakenya wengi wana hulka ya kuunga mkono maudhui chafu na kupuuza maudhui safi, basi Embarambamba anawafaa kabisa na hawafai kulalamika kwa vile anachokifanya ndicho kile wengi wanafurahia.

“Nimeona watu wakinitagi kwenye uwazimu wa Embarambara na mambo mengine kama hayo kwenye mitandao ya kijamii. Wakenya, mamlaka yangu si udhibiti tena. KFCB ni chombo kilichoidhinishwa na sheria kuhakiki na kuainisha maudhui. Hata hivyo, ninaamini kuwa Kenya inastahili Embarambara. Hatuthamini maudhui safi,” Mutua alisema kupitia Facebook.

Mkurugenzi huyo wa MCSK ambaye alifahamika Zaidi enzi za uongozi wake wa KFCB na misimamo yake mikali dhidi ya kazi zozote za Sanaa zenye maudhui ya kupotosha jamii aliilaumu jamii na kanisa pia kwa kupalilia maudhui chafu badala ya kuyakemea.

“Tunaonekana kutojali hata wakati yaliyomo ni ya kufuru. Makanisa na viongozi wa jumuiya huwa kimya wakati maudhui kama hayo yanapoongezeka. Natamani wasanii hawa wavue nguo na kutumbuiza kanisani hivyo hadi watupishe dhamiri!” aliongeza.

Baadhi ya Wakenya walimtaka Mutua kumkomesha Embarambamba muda mfupi baada ya msanii huyo kutoka Kisii kuachia kionjo cha wimbo wake ‘Tuko uchi mbele za Mungu’ akionekana kucheza densi bila nguo, Zaidi ya taulo pekee.