Zuchu si mchoyo, nikimuomba kitu chochote ananipa kwa wakati - Diamond Platnumz

Diamond alifichua kwamba sababu kuu ya kushindwa kumuacha Zuchu ni ukarimu wake, kwani mrembo huyo wa ‘Sukari’ hachelewi kumpa kitu chochote anachomuitisha, tena hufanya hivyo kwa wakati.

Muhtasari

• “Nampenda sana Zuchu kwa sababu ni mtu mkarimu hivyo nikimwomba kitu chochote, ananipa kwa wakati,” Diamond alisema.

Diamond na Zuchu
Diamond na Zuchu
Image: Instagram

Diamond Platnumz amefichua kwa nini penzi lake kwa Zuchu haliwezi likakauka licha ya songombingo katika uhusiano wao usiotabirika.

Akizungumza wakati wa shoo yao ya pamoja kisiwani Zanzibar, Diamond alisema kwamba anampenda Zuchu kupita kiasi hata kama mara kwa mara wawili hao wanatishiana kuachana kwa kuchapisha jumbe mitandaoni kwamba wako single na muda mchache baadae kuonekana wakila bata pamoja.

Diamond alifichua kwamba sababu kuu ya kushindwa kumuacha Zuchu ni ukarimu wake, kwani mrembo huyo wa ‘Sukari’ hachelewi kumpa kitu chochote anachomuitisha, tena hufanya hivyo kwa wakati.

“Nampenda sana Zuchu kwa sababu ni mtu mkarimu hivyo nikimwomba kitu chochote, ananipa kwa wakati,” Diamond alisema.

Msanii huyo anayetajwa kuwa mtumbuizaji bora kuwahi kutokea tangu ujio wa Bongo Fleva miaka ya 90 alisema kwamba ukarimu huo wa Binti Khadija Kopa ndio unaomfanya hata yeye kujitoa pakubwa kwake kama njia ya kurudisha mkono.

 “Ndio maana mimi huwa najinyima kwas ababu yake na Zanzibar nimekuja kwa ajili yake,” Diamond alisema.

Ifahamike Diamond alimfuata Zuchu kisiwani Zanzibar wikendi iliyopita baada ya mrembo huyo ambaye yuko chini ya lebo ya WCB Wasafi kuandika ujumbe mrefu kwenye Instagram kwamba amefanya uamuzi wa kumuacha Diamond baada ya maumivu ya kimapenzi kuzidi.

Zuchu alifunguka hayo muda mfupi baada ya video ya Diamond akiwa ameshikana mikono kimahaba na babymama wake Zari kuibuka mitandaoni.

Katika video hiyo, Diamond aliinukuu kuwa alikuwa akisherehekea wakati mzuri na ‘dada yake’ kwa maana ya Zuchu.

Hata hivyo, picha hiyo haikuacha upande wa pili salama maana inaarifiwa pia Shakib Cham, mpenzi wa Zari naye alifungasha virago na kuondoka zake kisa kumuona Zari akiwa na Diamond licha ya kuachana takribani miaka 5 iliyopita.