Mike Sonko adai kufilisika hadi kulazimika kutumia shilingi 1,700 tu kwenye kinyozi

“Siku hizi nimesota mpaka nanyolewa kwa kijiji. Kunyolewa, manicure, pedicure, facial na masaji vyote nafanyiwa kwa shilingi 1,700,” Sonko aliandik.

Muhtasari

• Mwezi Novemba mwaka 2022, Sonko pia alionekana kwenye kinyozi mmoja ambapo alidai kufilisika na kutaja bei ya kunyolewa hapo kuwa shilingi 300.

Mike Sonko
Mike Sonko
Image: Screengrab//X

Gavana wa zamani wa Nairobi, Mike Sonko amekiri kupitia ukurasa wake mtandaoni X kwamba amefilisika.

Sonko alipakia video akiwa kwenye kinyozi na kudai kwamba siku hizi amefilisika kiasi kwamba amelazimika kuanza kupata huduma ya kunyolewa kwenye vinyozi wa wastani.

Sonko alionekana akinyolewa kwenye kinyozi chenye hadhi ya wastani na mwanamke na kusema kwamba huduma zote kutoka kunyolewa hadi kufanyiwa masaji hazizidi shilingi elfu moja na mia saba.

“Siku hizi nimesota mpaka nanyolewa kwa kijiji. Kunyolewa, manicure, pedicure, facial na masaji vyote nafanyiwa kwa shilingi 1,700,” Sonko aliandika kwenye video hiyo.

Hata hivyo, uchunguzi wetu ulibaini kwamba hii si mara ya kwanza Sonko kudai kwamba amefilisika baada ya kuonekana akinyolewa katika kinyozi cha hadhi ya wastani.

Mwezi Novemba mwaka 2022, Sonko pia alionekana kwenye kinyozi mmoja ambapo alidai kufilisika na kutaja bei ya kunyolewa hapo kuwa shilingi 300.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa X kipindi hicho, alichapisha video yake akiwa kwenye kinyozi akinyolewa mtindo mpya wa nywele. Hata hivyo, mahali hapo palionekana penye hadhi ya chini si mahali ambapo ungetarajia mfanyabiashara huyo shupavu kuwa.

Aliendelea na kunukuu video hiyo, "leo nanyolewa kwa kinyozi cha 300/= Nitafuliza tu sahii (leo nanyoa nywele kwenye kinyozi cha bei nafuu kinachotoza 300/= tu mwisho wa yote naenda. kuchukua mkopo wa simu ili kulipa.)"

Licha ya kudai mara kadhaa kwamba amefilisika, Sonko amekuwa akionekana kuendeleza misaada yake kwa watu mbalimbali wenye ugumu kimaisha.