“Tafadhali tap-tap tufike 20k, nitumieni zawadi za maua na kofia” – Kanyari aomba mashabiki TikTok

“Nani alisema tiktok ni mbaya? Mimi nashangaa. Tiktok si mbaya, kama wahubiri wanasema tiktok ni mbaya basi hata wao wafunge TV,” Kanyari alimjibu aliyeandika kwamba pasta mmoja alisema mtu ako Tiktok hana maisha.

Muhtasari

• Mchungaji huyo pia alisikika akiwarai mashabiki wake kuendelea ku’tap-tap’ akisema kwamba wamo safarini kufikisha wafuasi elfu 20 kutoka elfu 10 ambao walikuwa kipindi anaenda ‘live’.

MCHUNGAJI VICTOR KANYARI
MCHUNGAJI VICTOR KANYARI
Image: MAKTABA

Siku chache baada ya kutangaza kujiunga kwenye jukwaa la video la TikTok, mchungai Victor Kanyari sasa ni mtu mwenye furaha baada ya kupata mapokezi ya aina yake na mashabiki wa mtandao huo.

Kanyari katika video moja inayopiga misele mitandaoni ambayo inamuonyesha akiwa mubashara, aliwashukuru mashabiki wake kwa kumwezesha kupata idadi kubwa ya wafuasi chini ya siku chache.

Mchungaji huyo pia alisikika akiwarai mashabiki wake kuendelea ku’tap-tap’ akisema kwamba wamo safarini kufikisha wafuasi elfu 20 kutoka elfu 10 ambao walikuwa kipindi anaenda ‘live’.

Kanyari pia alionyesha furaha yake baada ya kutumiwa zawadi mbali mbali kama kofia na maua na bunduki.

Ikumbukwe katika mtandao huo, zawadi hizo hugeuzwa kuwa pesa baadae na mtu anaweza kuzitoa na kuzitumia.

“Tap-tap tufike elfu 20, tulikuwa tumefika hiyo ya kwanza elfu 30 lakini sasa tuko elfu 10. Tafadhali tap-tap tufike 20,000,” Kanyari alionekana akitoa rai kabla ya kuvutiwa na baadhi ya jumbe za wafuasi wake.

Licha ya baadhi kuonekana kumuunga mkono, baadhi pia walionekana kumkashifu kwa kutumia mtandao huo unaojulikana nchini kwa hulka ya watumizi wake kuwa na maneno machafu.

Hata hivyo, Kanyari aliwapuuzilia mbali wale wanaomsimanga akisema kwamba anayesema tiktok ni mbaya basi hata TV hafai kutazama.

“Ahsante, endeleeni kutap-tap. Wale wanaongea vibaya wacha waongee vibaya, lakini mimi nimeamini kwamba kuna watu wako hapa wanataka maombi, wanataka kubarikiwa, wanataka mambo mazuri,” Kanyari alisema.

“Nani alisema tiktok ni mbaya? Mimi nashangaa. Tiktok si mbaya, hata TV basi ni mbaya, kama wahubiri wanasema tiktok ni mbaya basi hata wao wafunge TV,” Kanyari alimjibu mmoja aliyeandika kwamba pasta mmoja wa humu nchini alisema mtu ako Tiktok hana maisha.

Mchungaji huyo pia aliwarai wafuasi wake kando na kutap-tap, waendelee kumtumia zawadi, akionesha furaha yake baada ya kupokea zawadi nyingi za maua na kofia.

“Ahsante sana, wow ndio hiyo kofia, nakushukuru kwa kunitumia kofia. Nitumie maua, nitumie bunduki na Mungu awabariki,” kanyari alisema huku akipiga funda la kinywaji na kuthibitisha kwa watazamaji wake akisema, “Hayo ni maji halisi.”