Tazama baadhi ya mambo yenye utata ambayo mapasta wa Kenya waliwahi kufanya

Kando na askofu Johanna, watumishi wa Mungu wengine kadhaa wa Kenya wamevuma sana kutokana na mambo yenye utata.

Muhtasari

•Johanna alianza kuvuma mapema wiki hii baada ya video ambayo inamuonyesha akipaka mafuta kwenye sehemu mbalimbali za mwili mwanamke.

•Hata hivyo, askofu Johanna sio mtumishi wa Mungu pekee Mkenya ambaye matendo yake yaliibua gumzo mitandaoni.

Mhubiri James Ng'ang'a, Bishop Johanna na Paul MacKenzie
Image: HISANI

Mwanaume anayedaiwa kuwa mtumishi wa Mungu, Danson Gichuhi almaarufu Askofu Johanna amekuwa akivuma sana kwenye mitandao ya kijamii katika siku mbili zilizopita kutokana na njia yake maalum ya 'kutoa mapepo.'

Johanna alianza kuvuma mapema wiki hii baada ya video ambayo inamuonyesha akipaka mafuta kwenye sehemu mbalimbali za mwili mwanamke aliyelala chali kusambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Katika video hiyo, mtumishi huyo wa Mungu alisikika akimwombea mwanamke huyo huku akiendelea kumpaka mafuta mwilini.

Katika video nyingine ambayo imekuwa imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii, mchungaji Johanna anaonekana akimuombea mwanamke asiyetambulishwa ambaye alidaiwa kuwa na mapepo. Johanna anasikika akiyaamuru mapepo hayo kumtoka mwanamke huyo na hata kutumia nguvu kuyaamuru yatoke.

Aidha, anasikika akiongea na ‘mapepo’ hayo huku akimpiga makofi mwanamke huyo kwenye sehemu tofauti za mwili ikiwamo tumboni, miguuni na makalio.

Matendo yake ‘akitoa pepo’ kutoka kwa wanawake kwa njia ya kutatanisha zimeendelea kuibuka kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, askofu Johanna sio mtumishi wa Mungu pekee Mkenya ambaye matendo yake yaliibua gumzo mitandaoni.

Chini hapa tazama baadhi ya mambo mengine yenye utata ambayo baadhi ya mapasta wa Kenya walifanya;-

  • Askofu Johanna alimpaka mwanamke mafuta kwenye matiti, sehemu za siri: Video za kushangaza  za mchungaji huyo akitoa mapepo kutoka kwa wanawake kwa njia za kutatanisha zimevuma sana mwezi huu wa Februari 2024.
  • Paul Mackenzie aliwaomba waumini wasikule hadi wafe: Mtumishi huyo mwenye utata ambaye kwa miaka kadhaa alikuwa akiendesha katika kanisa la Good News International Church katika eneo la Shakahola, kaunti ya Kilifi alikamatwa mwaka jana baada ya kuhusishwa na maovu kadhaa ikiwamo mauaji ambapo anadaiwa kuwaagiza waumini kujinyima chakula hadi wafe.
  • Eliud Wekesa almaarufu ‘Yesu wa Tongaren’ alidai kuwa Yesu Kristo: Mchungaji huyo mwenye utata alivuma katikati mwa mwaka wa 2023 baada ya kujitokeza hadharani akidai kwamba yeye ndiye Bw Yesu.
  • Charles Wanyonyi almaarufu ‘Yehova Wanyonyi’ alidai kuwa mungu:Ukweli kuhusu iwapo amekufa kama ilivyoripotiwa na mamlaka au bado yupo hai bado umebaki kuwa  kitendawili lakini Bw Wanyonyi alivuma sana kabla ya mwaka wa 2015 baada ya kuibuka akijidai kuwa Mungu.
  • James Ng’ang’a aliwaonya wenye shahada kutohudhuria kanisa lake: Mhubiri James Nganga amekuwa kwenye habari mara nyingi huku akilengwa kutokana na utata mwingi uliozingira kazi yake. Mwaka jana, aliwaonya wenye shahada dhidi ya kuhudhuria kanisa lake akisema wana ujuzi mdogo wa neno la Mungu.
  • Paul MacKenzie alikamatwa kwa kuwahimiza watoto wasiende shule: Mwaka wa 2017 na tena 2018, alikamatwa kwa madai ya kuhimiza watoto wasiende shule huku akidai kuwa elimu haitambuliwi katika Bibilia.
  • Victor Kanyari aliwauzia waumini miujiza kwa Ksh310: Hivi majuzi mhubiri Victor Kanyari alikiri kwamba alikuwa akiwashinikiza waumini kutoa mbegu ya 310 kwa ajili ya maombi kama njia ya yeye kukwepa ufukara.
  • Gilbert Deya alishtakiwa kwa kuiba watoto mwaka wa 2006.

Chanzo: Majarida ya Kenya