Video zingine za Askofu Johanna 'akiwatoa pepo' wanawake kwa njia za kutatanisha zaibuka

Video nyingine inamuonyesha askofu huyo akimpiga mwanamke tumboni, miguuni na makalioni huku ‘akimtoa mapepo’.

Muhtasari

•Video zingine za  Askofu Johanna ‘akitoa pepo’ kutoka kwa wanawake kwa njia ya kutatanisha zimeendelea kuibuka kwenye mitandao ya kijamii.

•Katika video nyingine, Askofu Johanna anaonekana akimwombea mwanamke mwingine ambaye anaonekana akiwa amelala chini.

'akitoa mapepo' kwa wanawake.
Bishop Johanna 'akitoa mapepo' kwa wanawake.
Image: HISANI

Video zingine za mchungaji mwenye utata Danson Gichuhi almaarufu Askofu Johanna ‘akitoa pepo’ kutoka kwa wanawake kwa njia ya kutatanisha zimeendelea kuibuka kwenye mitandao ya kijamii.

Imebainika kuwa mtumishi huyo wa Mungu ambaye mara nyingi ameonekana akiwa amevalia vazi refu jekundu na kilemba kichwani amekuwa akichapisha video za vipindi vyake cha ‘kutoa mapepo’ kwenye akaunti yake ya tiktok, @bishop.johanna.

Katika video nyingine ambayo imekuwa ikivuma kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, askofu Johanna anaonekana akimuombea mwanamke ambaye hajatambulishwa ambaye alidaiwa kuwa na mapepo. Johanna anasikika akiyaamuru mapepo hayo kumtoka mwanamke huyo na hata anaonekana akitumia nguvu kuyaamuru yatoke.

Katika video hiyo ambayo imewaacha wanamitandao wengi kwa mshangao na mshtuko, mchungaji huyo mwenye utata anasikika akizungumza na ‘mapepo’ yaliyomshika mwanamke huyo huku akimpiga makofi sehemu tofauti za mwili ikiwamo tumboni, miguuni na makalio.

“Mimi nakumaliza, mimi nakumaliza saai. Wee Msoo, si ata wewe unawamaliza. Utawafungua wote?” mchungaji anasikika akimwambia mwanamke huyo.

Kisha anaonekana akimwamuru mwanamke huyo kubingiria chini na kupiga nduru kabla ya kumuombea kwa lugha ya Kikuyu.

Katika video nyingine, Askofu Johanna anaonekana akimwombea mwanamke mwingine ambaye anaonekana akiwa amelala chini. Anaonekana kumpiga kofi usoni huku akipiga gumzo naye

Mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mama Shiro kisha anasikika akipiga nduru kana kwamba ana maumivu huku mtumishi huyo wa Mungu mwenye utata akiamuru mapepo yaondoke.

Askofu huyo ambaye kwa sasa amefuta video nyingi kwenye akaunti yake ya mtandao wa tiktok ameendelea kuzua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii huku watumiaji wa mitandao wakijiuliza iwapo kanisa lake linafuata mafundisho halisi ya kibiblia au ana ajenda nyingine.

Johanna amekuwa alianza kuvuma takriban siku mbili zilizopita baada ya video inamuonyesha akipaka mafuta kwenye sehemu mbalimbali za mwili mwanamke aliyelala chali kusambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Katika video hiyo, mtumishi huyo wa Mungu alisikika akimwombea mwanamke huyo huku akiendelea kumpaka mafuta mwilini.

Katika mahojiano na Kururia TV, Johanna alifichua kwamba ni mwanamke huyo aliyemtafuta ili amsaidie kukabiliana na masuala ya ndoa ambayo alikuwa akikabiliana nayo.

"Video ilichukuliwa Ijumaa. Mwanamke huyo alikuwa ametoka Nairobi. Alikuja na matatizo mengi ya ndoa. Mumewe alikuwa ametoroka na kumuacha na watoto watatu. Mumewe alikuwa amechukuliwa na mwanamke mwingine. Mwanaume huyo angerudi nyumbani mchana na baadaye kwenda tena,” Askofu Johanna alisimulia

Aliongeza. “Mume wake alipoenda sana, mwanamke huyo aliona namba yangu na kunipigia. Aliniambia kuwa anataka kuja kanisani kwangu ili niweze kumhudumia. Alipokuja nilimhudumia, niliona shida alizonazo (kawaida huwa naona shida za watu). Nikamwambia kuna mwanamke anayeitwa ‘Carol’ amemchukua mumewe. Carol ndiye mwanamke aliyempokonya mume wa mwanamke huyo. Bibi huyo anaitwa Wanjiru."

Huku akitetea mtindo aliotumia kufukuza mapepo, Johanna alitumia mstari wa Biblia kuhusu uhitaji wa mgonjwa kutafuta wazee wa kanisa ili wawapake mafuta kwa ajili ya uponyaji.