Diamond ataja sababu zinazomzuia kuzungumzia kesi ya P Diddy

Diamond alimtaja rapa huyo wa Marekani kama rafiki wa karibu ambaye aliwahi kumkaribisha nyumbani kwake kipindi cha ziara yake USA. P Diddy kwa sasa anatuhumiwa na makumi ya kesi za unyanyasaji kingono.

Muhtasari

• P Diddy amekuwa chini ya uchunguzi kwa wiki kadhaa sasa baada ya watu mbalimbali kujitokeza na kudai kwamba amewahi wadhulumu kingono.

Image: hisani,

Gwiji wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz kwa mara ya kwanza amevunja kimya chake kuhusu kesi za unya yasaji wa kingono ambazo zinamuandama rapa wa Marekani, P Diddy.

 

Akizungumza na waandishi wa habari za burudani wakati wa kutangaza tamasha la muziki litakalofanyika baadae mwezi huu, Platnumz alisema kwamba P Diddy ni rafiki yake na kuna vitu vingi tu ambavyo vinamzuia kuzungumzia kesi hiyo ambayo imekuwa ikichunguzwa kwa muda sasa.

Diamond alikumbuka jinsi P Diddy aliwakaribisha nyumbani kwake miaka ya nyuma yeye na timu yake walipokuwa na ziara ya Marekani.

Alisema kwamba tuhuma hizo zinazomkabili Diddy zinakaa kisheria Zaidi na hivyo asingeweza kuzizungumzia hadi pale wachunguzi wakamilishe uchunguzi wao.

“Kwanza kabisa nisingependa kujifanya mchambuzi sana kwenye tukio lake kwa sababu sijazomea sheria. Kwa hiyo kwa ukweli ni mpaka mahakama au mamlaka zao zitakaposema hapo... lakini siwezi sema nimhukumu au nimkatalie hapana.”

“Lakini nashukuru Mungu katika moja ya ziara zangu za Marekani tulienda mimi na Babu Tale na Swizz Beatz, alitualika kwake tukapata chakula pale nini, unajua kulikuwa na familia yake, watoto na wasanii wake wapya kwa hiyo, alinishauri kidogo kwenye muziki, licha ya kwamba kuna vitu vyovyote wao watakavyozungumza lakini mimi nilimheshimu kama msanii, na mtu ambaye katika muziki anajua vitu vingi sana,” Diamond alimkingia kifua P Diddy.

P Diddy amekuwa chini ya uchunguzi kwa wiki kadhaa sasa baada ya watu mbalimbali kujitokeza na kudai kwamba amewahi wadhulumu kingono.