“Ni unga tunatafuta!” Mtumba Man amtetea Kinuthia, Burale akimtaka kuacha mavazi ya kike

“Burale haelewi ni unga tunatafuta, nikitoa sketi atanilisha na Kinuthia?” Mtumba Man aliuliza kwenye video hiyo akicheza densi kwa ngoma ya Ohangla.

Mtumba Man amtetea Kinuthia kwa Burale
Mtumba Man amtetea Kinuthia kwa Burale
Image: Maktaba

Cross-dresser Mtumba Man amemtetea tiktoker mwenzake Kelvin Kinuthia ambaye pia ni maarufu kwa kuvaa mavazi kinyume na jinsia yake baada ya mshauri wa kimaisha Robert Burale kumzomea akimtaka kuacha kuvaa kama mwanamke hali ya kuwa yeye ni mtoto wa kiume.

Kupitia kwa akaunti yake ya TikTok, Mtumba Man, ambaye huvaa kama mwanamke katika kile alisema kuwa ni mbinu ya kuwavutia wateja kwa biashara yake ya kuuza nguo za wanawake, alimjibu Burale akisema Kinuthia kuvaa nguo za kike haimaanishi kwamba ni wa ule mrengo mwingine bali ni riziki tu anatafuta unga.

“Burale haelewi ni unga tunatafuta, nikitoa sketi atanilisha na Kinuthia?” Mtumba Man aliuliza kwenye video hiyo akicheza densi kwa ngoma ya Ohangla.

Mtu huyo wa Mungu alikuwa amehoji ni kwa nini Kinuthia alikuwa amevalia nguo za kike na kutamba kwenye mitandao ya kijamii licha ya kuwa yeye ni mwanamume.

"Pia anahitaji kufundishwa. Kwa nini avae kama mwanamke, akicheza kwenye mitandao ya kijamii? Anahitaji kuambiwa ukweli. Huwezi kwenda kufanya twerking, na wewe ni mwanaume. Anahitaji kuambiwa ukweli," Burale alisema katika shoo ya Obinna kwenye YouTube siku chache zilizopita.

Kisha Burale alimuonya Obinna kwa ukali kumwambia Kinuthia avae kama mwanamume ikiwa kweli alikuwa anakuja kwa onyesho na karibu naye.