Ujumbe wa Sonko kwa wanaokejeli Njugush na mkewe kujitosa kwenye biashara ya matatu

" Kuna Mungu mbinguni na shetani daima ni mwongo. Najua watafanikiwa,” Sonko alisema.

Njugush na mkewe wanunua gari
Njugush na mkewe wanunua gari
Image: HISANI

Mjasiriamali na mwanasiasa Mike Sonko ametuma ujumbe wa kumpa hongera muigizaji Njugush na mkewe, wiki moja baada ya wanandoa hao kujitosa mazima katika biashara ya uchukuzi wa umma nchini.

Njugush na mkewe waliweka wazi kwamba waliuza gari aina ya Prado TX wailokuwa wakimiliki na kuwekeza pesa hizo katika ununuzi wa basi la abiria 33 na kulisajili kwenye sacco moja maarufu jijini Nairobi na viunga vyake.

Wakati mashabiki wao wengi walionekana kuwashabikia kwa jumbe za hongera, baadhi walionekana kuwasuta wakisema kuwa biashara yao haitadumu.

Sonko amewapa moyo Njugush na mkewe akisema kuwa hata yeye wakati alikuwa anaanza biashara sawia, maneno mengi yalisema lakini miaka michache baadae walifanikiwa.

Sonko alitabiri kwamba Njugush na mkewe watafanikiwa katika biashara ya sekta ya matatu jijini Nairobi, akiwasuta wanaosema biashara yao itabuma.

“Nimeona wenye chuki wachache wakijaribu kuwakatisha tamaa. Hata sisi tuliambiwa hatutaweza tulipoanza lakini tulishinda. Angalia tu, wanandoa hawa watathibitisha watu wengi wamekosea! Kuna Mungu mbinguni na shetani daima ni mwongo. Najua watafanikiwa,” Sonko alisema.

Wiki iliyopita, wanandoa hao walinunua basi dogo la abiria 33 na kulipatia jina la mtoto wao wa kwanza wa kiume, Tugi.

Kama sehemu ya uzinduzi, Super Metro ilitoa usafiri wa bila malipo kwa wateja wao wakiwaalika kwenye safari yao mpya. Walitangaza habari hizo za kusisimua kupitia mitandao yao ya kijamii.