Diamond ajibu tetesi za Alikiba kukwapua wafanyikazi wake kutoka Wasafi kwenda Crown Media

Diamond alisema kwamba hadhani kama ni vibaya mfanyikazi kuondoka kituo kimoja cha habari na kwenda katika kituo pinzani, kwani lengo la kila mtu ni kujiboresha kimaisha.

Muhtasari

• Alikiba hata hivyo, katika uzinduzi wa kituo hicho cha redio na runinga, alisisitiza kwamba itakuwa ni ya kujali maslahi ya kila mtu na wala si kujali maslahi ya mtu binafsi.

mwaliko wa Diamond.
Alikiba amekataa mwaliko wa Diamond.
Image: INSTAGRAM

Kwa mara ya kwanza, Diamond amezungumzia tetesi ambazo zimekuwa zikizagaa katika mitandao ya kijamii kuhusu Alikiba kulenga kumchukulia baadhi ya wafanyikazi wake kwenye shirika lake la habari la Wasafi Media na kuwapa ajira katika Crown Media.

Akizungumza na waandishi wa habari, Diamond aliulizwa kuhusu tetesi hizo na kutema nyongo akisema kwamba hadhani kama ni vibaya mfanyikazi kuondoka kituo kimoja cha habari na kwenda katika kituo pinzani, kwani lengo la kila mtu ni kujiboresha kimaisha.

Mkurugenzi huyo wa Wasafi Media alisema kwamba mtu anapoamua kugura kituo kimoja kwenda kingine ni Dhahiri ameitiwa ofa nzuri, na hakuna mtu katika utimamu wake wa kiakili anaweza kata hilo kani kila mmoja analenga maisha mazuri.

“Ukiona mtu anataka kutoka sehemu moja kuelekea nyingine basi atakuwa ameitiwa ofa nzuri, na hilo ni jambo zuri kwa sababu mimi napenda kuona mtu akipiga hatua nyingine na kujiendeleza maishani. Sioni tatizo mtu akitoka Wasafi Media na kujiunga na Crown Media,” Diamond alisema.

Itakumbukwa Crown Media inayohusishwa na Alikiba ilizinduliwa miezi michache iliyopita na kuja kwa kasi ya kipekee kwa kuwanyakua baadhi ya wanahabari kutoka vituo mbalimbali vikiwemo EFM, Clouds na vingine.

Alikiba hata hivyo, katika uzinduzi wa kituo hicho cha redio na runinga, alisisitiza kwamba itakuwa ni ya kujali maslahi ya kila mtu na wala si kujali maslahi ya mtu binafsi.

Hilo limekuwa likidhihirika wazi kutokana na jinsi Crown FM imekuwa ikicheza nyimbo hadi zile za wapinzani wa Alikiba, wakiwemo wasanii kutoka Wasafi WCB na Konde Music Worldwide.