Seneta Boni Khalwale asherehekea bintiye kufuzu kutoka chuo kikuu kama mhandisi

Watu walimtania Khalwale kwa kile walidai kwamba ana ukoo mpana ambao kila mara kama si kusherehekea kuzaliwa kwa mmoja wao basi n kusherehekea kupita mitihani ya kitaifa na kufuzu chuo.

Boni Khalwale na bintiye
Boni Khalwale na bintiye

Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale ni baba mwenye furaha na fahari baada ya bintiye kuhitimisha masomo yake ya chuo kikuu.

Kupitia ukurasa wake wa X, seneta huyo ambaye si mgeni kwa kusherehekea mafanikio ya wanafamilia wake alichapisha picha ya bintiye kwa jina Linda Lichuma na kufichua kwamba amefuzu kama mhandisi kutoka chuo kikuu cha Nairobi.

Khalwale alishukuru chuo hicho kwa kumpa maarifa ya kudumu binti yake katka fani ya uhandisi katika kipindi cha miaka 5.

“Napenda kutoa shukrani zangu za pekee kwa Chuo Kikuu cha Nairobi kwa kuelimisha, kufunza, kuchunguza, na kufuzu binti yangu, LINDA LICHUMA KHALWALE, katika kipindi cha miaka 5 iliyopita, ambaye leo amepata digrii ya Upper Second Honours katika Uhandisi. Kwa Mungu, mambo yote mazuri yanawezekana!” Khalwale alisema.

Itakumbukwa mwaka 2018, Khalwale alimsherehekea binti huyo kwa kufuzu kutoka shule ya kitaifa ya wasichana ya Alliance kwa alama ya A.

Hata hivyo, baadhi ya watumizi wa mtandao wa X walimtania Khalwale kwa kile walidai kwamba ana ukoo mpana ambao kila mara kama si kusherehekea kuzaliwa kwa mmoja wao basi n kusherehekea kupita mitihani ya kitaifa na kufuzu chuo.

“Watoto wa bonnie kila time ni kujoin nursery,kumaliza high school na ku graduate,kwani uji power yake ni imported?” Odogwu.

“Khalwale ni baba wa vizazi vingi,”Kiptoo alisema.

Hata hivyo, wapo wengine waliomuomba seneta huyo kuwapa ridhaa ya kuoa binti yake.