Maseneta waidhinisha kutimuliwa kwa naibu gavana wa Kisii Robert Monda

Monda alipatikana na hatia katika makosa yote manne, huku maseneta 39 wakipiga kura ya ndiyo kwa shtaka la ukiukaji mkubwa wa katiba.

Muhtasari

• "Seneti imeazimia kumuondoa afisini kwa kumtimua Robert Monda, Naibu Gavana wa Kisii, na sasa ataacha kushikilia wadhifa huo mara moja." Alitangaza Spika Amason Kingi.

Robert Monda akisubiri kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi yake katika bunge la Seneti mnamo Machi13 2024/ Picha: EZEKIEL AMING'A
Robert Monda akisubiri kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi yake katika bunge la Seneti mnamo Machi13 2024/ Picha: EZEKIEL AMING'A

Maseneta walipiga kura kumuondoa Naibu Gavana wa Kisii, Robert Monda afisini Alhamisi jioni.

Monda alipatikana na hatia katika makosa yote manne, huku maseneta 39 wakipiga kura ya ndiyo kwa shtaka la ukiukaji mkubwa wa katiba na sheria zingine.

Kuhusu shtaka la matumizi mabaya ya ofisi, Maseneta 39 walipiga kura ya ndio, 3 walipiga kura ya kumuunga mkono, na mmoja hakupiga kura, huku Maseneta 35 walipata DG na hatia ya utovu wa nidhamu, na watatu pekee walipiga kura kumwokoa.

Monda pia alishindwa katika shtaka la nne, huku maseneta 34 wakimpata na hatia ya kufanya uhalifu.

"Seneti imeazimia kumuondoa afisini kwa kumtimua Robert Monda, Naibu Gavana wa Kisii, na sasa ataacha kushikilia wadhifa huo mara moja." Alitangaza Spika Amason Kingi.

Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale, ambaye pia kiranja wa wengi, aliwasilisha hoja ya kumshtaki Monda, akisema kuwa, ingawa madai ya uhalifu huo hayajathibitishwa kikamilifu, naibu gavana huyo huenda alipokea hongo.

“Tutakuwa tunajidanganya kuwa huyo kijana hajathibitisha kuwa alimtumia Naibu Gavana pesa, tutakuwa tunajidanganya tukipuuza ushahidi wa hao wanawake wawili, na tutakuwa tunadanganya nchi tukisema DG hakupokea pesa hizo.” Khalwale alisema.

Seneta wa Migori Eddy Oketch alisikitika jinsi mamilioni ya vijana walivyo na uwezo wa kufanya kazi lakini wanachanganyikiwa wanapoombwa hongo.

"Huenda nisijue kama Naibu Gavana ana hatia au la, lakini najua kuwa kura ya leo itakuwa ya mamilioni ya vijana wanaohangaika kusaka, walio na ujuzi, uwezo na nia ya kufanya kazi, lakini wanalazimika kutoa rushwa.” Oketch Alisema.

 Seneta Maalum Gloria Orwoba aliwataka wenzake kumpigia kura Naibu Gavana badala ya kubaki bila maamuzi.  “Nilipoangalia ushahidi wa Shilingi laki mbili kupelekwa kwa meneja aliyetakiwa kutoa kazi, nilijua huo ndio upanga ambao ungemzamisha naibu gavana. Orwoba alisema. 

Bunge la kaunti ya Kisii lilikiwa limepiga kura ya kumuondoa ofisini Naibu Gavana Robert Monda, kabla ya kuwasilisha hoja hiyo kwenye seneti kuambatana na sheria. Monda sasa ana fursa ya kwenda Mahakamani kujaribu kubatilisha uamuzi huo.