Fahamu sifa za 'Kienyeji' anayetafutwa na Daddy Owen kuwa mkewe

"Awe katika miaka ya 20 au 30," alisema.

Muhtasari

•Daddy Owen aliweka wazi kuwa hataki msichana wa mjini akidai kuwa wasichana wa mjini mara nyingi huwa wajuaji sana.

Owen alidokeza kuwa baadhi ya wanadada Wakenya tayari wameanza kujipendekeza kwake.

Image: INSTAGRAM// DADDY OWEN

Mwimbaji wa nyimbo za injili Owen Mwatia almaarufu Daddy Owen ameweka wazi kwamba yupo tayari kujitosa kwenye ndoa nyingine.

Owen na mkewe wa kwanza Farida Wambui walitengana mwishoni mwa mwaka wa 2020 baada ya kuwa pamoja kwa zaidi ya miaka mitatu kutokana na masuala ya kutokuwepo kwa uaminifu katika ndoa.

Mwanamuziki huyo mkongwe amesema sasa anatafuta msichana wa kijijini almaarufu 'Kienyeji' wa kuoa.

"Nataka mwanamke kienyeji mweusi kabisa, mcha mungu, wa kijijini kabisa," alisema katika mahojiano na stesheni moja ya  redio ya humu nchini.

Daddy Owen aliweka wazi kuwa hataki msichana wa mjini akidai kuwa wasichana wa mjini mara nyingi huwa wajuaji sana.

Alisema yuko tayari kumfundisha mke wake kutoka kijijini na kumweka sawa asije akachepuka akionja maisha mjini.

"Awe katika miaka ya 20 au 30," alisema.

Kwenye mtandao wa Instagram, Owen alidokeza kuwa baadhi ya wanadada Wakenya tayari wameanza kujipendekeza kwake.

"Nilisema mwanamke mweusi, watu wanakuja inbox na ati melanin.. ukishasema melanini wewe si kienyeji," alisema.

Katika mahojiano ya awali na Word Is, Owen alifichua hofu yake kwamba umri wake unasonga na bado hajapata familia yake.

Mwimbaji huyo wa injili alisema kwamba mama yake anamshinikiza atafute mtu wa kuwa anamtembelea naye.

“Ananiambia hata angalau niajiri mtu ili tu niache kutembea peke yangu nyumbani,” alisema.

"Ana wasiwasi kwamba ninaishi peke yangu, natembea peke yangu."

Owen, 40, alisema kuwa kufikia sasa alitazamia kuwa amemaliza kupata watoto.

"Sijajiandaa kwani naelewa sio uamuzi wangu peke yangu, nahitaji kuwa na mtu." Owen alisema kuwa hata akiwa na pesa, hajakamilika.

Alipoulizwa ikiwa anachumbiana, alisema bado anahofia kuwa huenda asifanye vyema baada ya ndoa yake ya kwanza kuvunjika.

"Hatua yoyote na mtu mwingine kunaweza kuleta kumbukumbu za maisha yangu ya nyuma. Najiuliza kama, nitamtendea vizuri au nitakuwa chini ya shinikizo sawa na mahusiano yakaisha tena?"

Alfichua kuwa sababu kuu ya yeye kutembea na kuendesha miradi vijijini mara kwa mara ni kutafuta mke.