Mwanamke wa West Pokot aliyekiri hajawahi kwenda mbali na nyumbani atafutwa ili kutimiziwa ndoto

Milka aliweka wazi anatamani kuzuru Kitale na Nairobi ili kuona jinsi watu wanavyoishi huko.

Muhtasari

•Milka Cheyech alizungumza kuhusu ndoto yake ya kusafiri mbali na eneo la nyumbani ili kuona jinsi sehemu zingine za nchi zilivyo.

•Zaunguka Africa ilisema timu yake inadhamiria kumpa safari salama, ya starehe na yenye maarifa anapogundua maeneo mapya.

aliweka wazi anatamani kuzuru Kitale na Nairobi ili kuona jinsi watu wanavyoishi huko.
Milka Cheyech aliweka wazi anatamani kuzuru Kitale na Nairobi ili kuona jinsi watu wanavyoishi huko.
Image: SCREENGRAB// NTV

Kampuni ya utalii ya Zunguka Africa Tours and Travel inamtafuta mwanamke kutoka kaunti ya Pokot Magharibi, Milka Cheyech, ambaye alizungumza kuhusu ndoto yake ya kusafiri mbali na eneo la nyumbani ili kuona jinsi sehemu zingine za nchi zilivyo.

Milka ambaye ni mkazi wa eneo la Katilok alivuma mitandaoni baada ya kuhojiwa na runinga ya NTV ambapo alikiri kwamba hajawahi kusafiri mbali na nyumbani. 

Katika mahojiano hayo, mwanamke huyo wa umri wa makamo alifichua kwamba mahali pa mbali zaidi aliwahi kusafiri ni Kesegon katika eneo bunge la Cherangany.

“Tangu nizaliwe sijafika hata Kitale, mwisho wangu ni Kesegon. Wakati naenda hiyo kibarua, ninaenda nisanye nguo, ile kuukuu, nisanyie hawa watoto. Hiyo ndo mwisho wangu, sijawahi kwenda mbali,” Milka alisema.

Aliongeza kuwa wanafamilia wake wengine pia wanatoka eneo ambako anaishi na akafichua kwamba yeye husafiri tu kuwatembelea au kwenda sokoni.

Milka alisema ana ndoto ya kusafiri hadi mji wa Kitale na jijini Nairobi siku moja, na akaomba usaidizi wa kufika huko.

“Ningependa tu ata angalau nianzie Kitale, hapo tu. Alafu niende Nairobi. Niende niangilie vile watu wanakaa huko, maisha ya huko iko namna gani. Sababu kukaa hapa West Pokot bure, ata huwezi kujua watu wanaendelea vipi huko.

Huwezi jua maisha inaendelea aje huko. Natamani tu nifike huko,naskia watu wanasema ni dunia injini. Natamani kwenda Nairobi,” alisema.

Kampuni ya Zunguka Africa sasa inamtafuta mwanamke huyo, kwa lengo la kumsaidia kutimiza ndoto yake ya kusafiri nje ya eneo alikozaliwa.

"Zunguka Afrika ina heshima kutoa usaidizi wetu kwa Milka. Kwa sasa tunamtafuta ili tuweze kuratibu ofa maalum ya utalii inayolingana na maslahi ya Milka na kuhakikisha uzoefu wake ni wa kukumbukwa na unaoboresha,” Zunguka Africa alisema katika taarifa.

Kampuni hiyo ya utalii ilisema kwamba timu yake inadhamiria kumpa safari salama, ya starehe na yenye maarifa anapogundua maeneo mapya.

“Tunawaalika Wakenya wenzetu watusaidie kumfuatilia ili tuweze kumpa safari hadi Nairobi. Kwa pamoja, tutengeneze kumbukumbu zisizoweza kusahaulika na kuhamasisha kupenda kusafiri maishani,” walisema.

Katika mahojiano, Milka alidokeza kwamba angepigwa na butwaa sana ikiwa angezuru mji mkubwa kama Nairobi na Kitale.

“Sijawahi kufika Kitale. Mtu akiiongelea ama nione kwa TV, yaani naona nikienda huko nitapotea. Naona huko ni dunia injini, sio kama West Pokot vile naona. Ni ngumu, hakuna mwenye atawahi kupeleka, ata utaenda aje? Utaanzia wapi uende hadi huko? Na hakuna mtu wa familia, hakuna nani huko,” alisema.