"Wanawake wananipenda, nawapenda pia!" DJ Fatxo azungumzia madai ya kuwa shoga

Mwimbaji huyo wa Mugithi alisema alishangaa sana kwanini wanawake ambao amekuwa nao hawakujitokeza kumtetea.

Muhtasari

•Katika mahojiano, alisema madai  ya ushoga ni uvumi tu ulioanzishwa na kuenezwa na maadui zake ambao hakufichuliwa.

•Mwimbaji huyo wa nyimbo za Kikuyu mwenye umri wa miaka 27 aliweka wazi kuwa anawapenda sana wanawake na wanampenda pia.

DJ Fatxo ndani ya ofisi za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mwimbaji wa Mugithi Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo amejitenga mbali na kundi la wapenzi wa jinsi moja almaarufu LGBTQ.

Katika mahojiano na Mpasho, alisema madai  ya ushoga ni uvumi tu ulioanzishwa na kuenezwa na maadui zake ambao hakufichuliwa.

Alibainisha kwamba hata hajawahi kupatwa na wazo la kuwa mpenzi wa jinsia moja

"Sijawahi kuwa, sitawahi kuwa na mimi si wa LGBTQ," Fatxo alisema.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za Kikuyu mwenye umri wa miaka 27 aliweka wazi kuwa anawapenda sana wanawake na wanampenda pia.

"Kuhusu kuwa mashoga, wanawake wananipenda na mimi nawapenda. Mimi sio shoga na siwezi," alisema.

Uvumi wa msanii huyo kuwa shoga uliibuka baada ya kuhusishwa na kifo cha Jeff Mwathi ambaye alifariki nyumbani kwake mwezi Februari.

Fatxo alikanusha madai ya kutumia mwanadada anayeaminika kuwa mpenzi wake kuficha kuwa yeye ni shoga huku akieleza mshangao wake kuhusu kwanini wanawake ambao amekuwa nao hawakujitokeza kumtetea.

"Ilikuwa ni jambo chungu zaidi kwangu(kuhusishwa na ushoga) kushinda mambo mengine mnaniwekelea kwa sababu nilitarajia wanadada wote ambao nimekuwa nao watokee waongee wanitetee waseme mimi sio shoga," alisema.

Kufuatia kifo chake, kulikuwa na madai kwamba marehemu Jeff Mwathi huenda alidhulumiwa kimapenzi kabla ya kudaiwa kuuawa, madai ambayo wanapatholojia walijaribu kuchunguza lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kupata majibu kwa sababu muda mwingi ulikuwa umepita tangu kifo chake. Sampuli za DNA zilichukuliwa kutoka kwa DJ Fatxo na washirika wake waliokuwa na marehemu kabla ya kifo chake  ili kusaidia uchunguzi huo.

Siku ya Jumatatu, mwimbaji huyo alisisitiza kwamba hakuhusika katika kifo cha kijana huyo ambaye alitambulisha kama rafiki yake.

"Jeff alikuwa rafiki yangu. Sioni sababu yangu kumuua," alisema.

Mamake Jeff Mwathi hata hivyo  alisisitiza kwamba bado anaamini mwimbaji huyo wa Mugithi alihusika.

"Hata yeye anafaa kupitia kitu kama hiyo. Alifanya vibaya sana, kuua mtoto wa mtu hivo hadharani," alisema.

Alilalamika kwamba haki haikutenda kwa mwanawe huku akipuuzilia mbali uchunguzi uliofanyiwa na DCI.