Mwanadada afungwa kifungo cha maisha jela kwa mauaji

Mahakama kuu Naivasha imemfunga mwanamke kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi wa chuo kikuu miaka 5 iliyopita.

Cecilia Waruguru Muriithi, 36 alishtakiwa kumuua mwanafunzi wa miaka 22 baada ya kugundua kuwa alikuwa anatoka kimapenzi na mmewe.

Jaji wa mahakama kuu Richard Mwongo alikataa ombi la kutomfunga mwanadada huyu kwa misingi kuwa uamuzi kama huo ungesababisha dhana potovu ya kutatua mizozo inayohusu mipango ya kando.

Upande wa mashtaka ulikuwa unashtaki kuwa Waruguru alihusika katika mauaji tarehe 30 Juni 2013 katika mtaa wa King'ori, eneo la Mai Mahiu kaunti ya Naivasha. .

Mwanafunzi huyu kwa jina Susan alikuwa ameajiriwa kama mfanyakazi katika boma la mwanamme wa mshukiwa wa mauaji. Jumbe zilizokuwepo kwenye simu ziliashiria waziwazi kuwa walikuwa katika mahusiano.

Mwili wa wake Susan ulipatikana umetupwa katika uwanja uliopo nje ya mjengo wa mwanamme huyo. Mwili ulikuwa na majeraha ya kudungwa visu na ulionekana kuchomeka kwa kumwagiwa maji moto au kemikali inayochoma ngozi.

Jaji alihukumu kuwa mauaji yalikusudiwa na kwa hivyo akatoa kifungo cha maisha kwa mshukiwa.

“Baada ya mauaji, mwili wa maiti ulitupwa katika uwanja hatua chache kutoka kwa nyumba yake. Huu ni ukatili na njama iliyopangwa kumuua mwendazake." alisema jaji.

Jaji alihoji kuwa mshukiwa wa mauaji ambaye ni mama wa watoto wawili hakuonyesha kuomba msamaha baada ya kupatikana na hatia. Alisema kuwa mwendazake alipitia maumivu makubwa yaliyopelekea kifo chake.

"Hivo basi namfunga kifungo cha maisha.Hukumu hii itaweza kurejelewa baada ya miaka 20 iwapo ataonyesha mabadiliko ya kitabia."

Hadithi imetafsiriwa na kuhaririwa na Abraham Kivuva