Jopo hilo litashughulikia kesi zote kuhusu kuvunjwa kwa bunge

Naibu Jaji Mkuu ateua jopo la majaji 5 kushughulikia kesi za kuvunjwa kwa bunge

Wabunge wamelaani ushauri wa Jaji mkuu kwa rais

Muhtasari
  •  Jopo hilo litaongozwa na jaji Lydia Achode
  • Majaji wengine ni  George Odunga, James Makau, Anthony Ndungu na  Pauline Nyamweya

 

Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu

 Naibu Jaji mkuu  Philomena Mwilu  ameliteua jopo la majaji watano ili kuzisikiza kesi kuhusiana na ushauri  wa jaji Mkuu  kwa rais Uhuru Kenyatta kulivunja bunge.

 Jopo hilo litaongozwa na jaji Lydia Achode.Majaji wengine ni  George Odunga, James Makau, Anthony Ndungu na  Pauline Nyamweya.

 Kuna kesi sita kuhusu ushauri huo wa Maraga kwa rais Uhuru

 Miongoni mwa kesi hizo ni ile ya wakenya wawili waliowasilisha ombi la kutaka mahakama kutupilia mbali ushauri wa jaji mkuu kwa rais. Bunge pia limemshtaki  Jaji mkuu David Maraga  na katika kesi nyingine  Mwanasheria mkuu Kiharaka Kariuki  amewasilisha ombi kupinga ushauri wa  Jaji mkuu kuhusu kuvunjwa kwa bunge.

 Bunge limesema kuvunjwa kwake sio jambo linalowezekana  kama alivyoshauri jaji mkuu. Bunge  limesema hatua hiyo ya Maraga ni kosa kubwa  na  halipo katika sheria.

  Wabunge wanasema iwapo rais atafuata ushauri wa Maraga basi misuada yote iliyoidhinishwa na rais kuwa sheria  kupitia wabunge  haitaweza kutekelezwa kwa sheria.

 Mwanasheria mkuu Kihara Kariuki  naye amesema iwapo bunge litavunjwa hatua hiyo itampa rais Muhula  mwingine.

 Muungano wa Third Way Alliance  nao pia una kesi ya kutaka mahakama itafisiri  katiba kuhusu suala la kulivunja bunge.

Chama cha mawakili nchini LSK hata hivyo kinaunga mkono ushauri huo wa Maraga. Rais wa LSK Nelson Havi wiki hii aliongoza mawakili kulitwaa bunge akisema kwamba wabunge kwa sasa wanahudumu kinyume na sheria.