Mhubiri amwua mkewe baada ya kupata ujumbe mfupi wa kimapenzi

crime scene
crime scene

Mhubiri mmoja kutoka Kisii aliyemnyonga mkewe hadi kufa kisha akajaribu kuficha ukweli wa kisa hicho kwa kumpeleka mkewe hospitalini na kudai kuwa alikunywa sumu amekamatwa.

Ripoti moja ya polisi imehusisha kisa hicho na ujumbe mfupi wa kimapenzi ambao mshukiwa huyo Joel Mogaka alipata kwenye simu ya mkewe. Mshukiwa huyo atasalia kizuizini polisi wanapokamilisha uchunguzi kabla ya kufikishwa mahakamani.

Ufuatao ni msururu wa habari kutoka nyanja mbalimbali nchini; 

Kuwa na urais wa mzunguko kutaunganisha nchi zaidi. Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli anasema madai ya naibu rais William Ruto na wandani wake kwamba kutachangia ukabila si ya kweli.

Anasema urais wa mzunguko utasaidia kuziunganisha jamii ambazo hazipatani na vile vile utazuia vita vinavyoshuhudiwa kila tunapokuwa na uchaguzi.

Zaidi ya wagombeaji 14 watawasilisha stakabadhi zao za uteuzi kwa tume ya uchaguzi IEBC ili kupewa idhini ya kugombea kiti cha uwakilishi wadi wa Huruma, Eldoret katika uchaguzi mdogo ambao utafanyika tarehe 4 Machi.

Miongoni mwao ni wagombeaji 6 huru.

Huenda ukaendelea kukosa huduma za kutosha za afya iwapo mgomo wa wahudumu wa afya utaendelea wiki hii. Spika wa Seneti Ken Lusaka sasa analitaka baraza la magavana kushirikiana na wafanyikazi wa afya kutafuta suluhu ya kudumu.

Baadhi ya wakaazi katika kijiji cha Mbela Ukunda wameachwa bila makao baada ya nyumba zao kubomolewa. Mbunge wa Msambweni Feisal Bader na Mwakilishi wadi wa Bongwe Gombato Hassan Matumizi  wanasema kuwa wakaazi hao hawakuwa wamepewa ilani ya kuondoka.