MGOGORO WA NDOA

Homabay: Polisi awindwa kwa kudunga sehemu za siri za mkewe baada ya kushuku anamcheza

Alishuku kuwa mkewe alikuwa anatoka nje ya ndoa baada ya kuchukua simu yake na kuangalia watu aliokuwa anazungumza nao

Muhtasari

•Familia ya mhasiriwa imeeleza kuwa mshukiwa alikuwa amerudi nyumbani kutoka kazini na kuchukua simu ya mkewe ili kuangalia watu ambao alikuwa anawasiliana nao akiwa kazini.

•Babake mhasiriwa, Alfeus Ongou amesema kuwa binti yake alijaribu kueleza bwana yake kuwa walikuwa wakizungumza kuhusiana na masomo ya wanao watatu ila bwanake ambaye ni afisa pande hizo  za Homabay hakutaka kuskia.

crime scene 1
crime scene 1

Maafisa wa polisi upande wa Homa Bay wanamtafuta mwenzao anayedaiwa kudhulumu mkewe baada ya kushuku kuwa alikuwa anamcheza na naibu mwalimu mkuu.

Inadaiwa kuwa mshukiwa alitumia kucha zake kudunga sehemu za siri za mkewe wakiwa nyumbani kwao katika kijiji cha maeneo ya Rachuonyo, Homabay.

Familia ya mhasiriwa imeeleza kuwa mshukiwa alikuwa amerudi nyumbani kutoka kazini na kuchukua simu ya mkewe ili kuangalia watu ambao alikuwa anawasiliana nao akiwa kazini.

Hapo ndipo alitilia shaka simu nyingi ambazo mkewe alikuwa anapigiana na mwalimu mmoja kutoka shule moja maeneo hayo ya Rachuonyo.

Babake mhasiriwa, Alfeus Ongou amesema kuwa binti yake alijaribu kueleza bwana yake kuwa walikuwa wakizungumza kuhusiana na masomo ya wanao watatu ila bwanake ambaye ni afisa pande hizo  za Homabay hakutaka kuskia.

Hapo na hapo akaanza kumpiga kabla ya kumdunga kwenye sehemu zake za siri kwa kutumia kucha zake.

"Nahofia kwa kuwa binti yangu amedhulumiwa vibaya. Mpaka alimdunga kwa kucha zake. Nahofia huenda akamuua"  Ongou alisema.

Kesi hiyo iliripotiwa katika kituo cha polisi cha Oyugis usiku huo kabla ya mhasiriwa kuenda kutibiwa katika hospitali ya Rachuonyo.

Naibu Kamishna wa kaunti, David Kiprop amelaani kitendo hicho na kukiita cha kikatili huku akiahidi kuwa mshukiwa atafunguliwa mashtaka punde baada ya kukamatwa. 

Kiprop alisihi walio kwenye ndoa kusuluhisha migogoro yao kwa njia ambayo haisababishi madhara kama vile kuhusisha wazee wa kijiji na wataalam wa kushauriana kuhusu mambo ya ndoa.