"Nimetumia aina zote za madawa ya kulevya" Babu Owino akiri

Amesema kuwa pombe ilimpatia nguvu ambayo alitumia vibaya

Muhtasari

•Hata hivyo, ameeleza kuwa hayo yalikuwa maisha yake ya awali na kwa sasa amebadilika. Amesema kuwa uraibu wa dawa za kulevya ulikuwa karibu kumharibia maisha.

•Babu ameitaka serikali kuhalalisha unywaji ya chang’aa, busaa na Muratina huku akisema kuwa ni pombe za kitamaduni na zinaongeza nguvu mwilini.

Babu Owino
Babu Owino
Image: Maktaba

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino ameshangaza Wakenya baada ya kufunguka kuhusiana na maisha yake ya awali alipokuwa amezama kwenye uraibu wa madawa ya kulevya.

Akizungumza na Robert Alai kwenye kipindi cha The Audit siku ya Jumanne, mbunge huyo amekiri kuwa aliwahi kuwa mwathiriwa mkubwa wa mihadarati aina nyingi tofauti.

Maishani mwangu hakuna mihadarati sijatumia. Nimetumia madawa laini na madawa nzito. Nimetumia bangi, nimetumia Cocaine, Heroine, nimetumia mihadarati aina nyingi. Nimekunywa aina zote za pombe” Babu alisimulia.

Hata hivyo, ameeleza kuwa hayo yalikuwa maisha yake ya awali na kwa sasa amebadilika. Amesema kuwa uraibu wa madawa ya kulevya ulikuwa karibu kumharibia maisha.

"Pombe huwa na  wanga  ambayo inapatia mwili nguvu. Niliwacha kutumia pombe kwani  ilinipa nguvu nyingi ambayo nilitumia vibaya" Babu alisema.

Amewaagiza vijana kuepukana na utumizi wa dawa za kulevya huku akisema kuwa zinadhuru afya.

“Madawa yoyote yale yanadhuru afya yako. Mwanzo yanaharibu viungo vya mwili kumaanisha maisha yako yatapunguzwa, pili fikra zako zinaathirika na kukupelekea kufanya maamuzi yasiyo mazuri. Kwa hivyo nawasihi msitumie mihadarati yoyote. Mimi mwenyewe nimetumia aina zote za madawa hayo ila sikuona manufaa yake” Babu alisema.

Babu ametaja msongo wa mawazo kutokana na ukosefu wa ajira na  shida za kifamilia kuwa sababu moja inayowapelekea vijana kutumia mihadarati wakitazamia kusahau shida zinazowakumba. Hata hivyo, ameeleza kuwa dawa zile zinafanya mtu asahau shida zake kwa muda tu kwani mawazo yale hurejea punde baada ya kurejesha fahamu.

“Kabiliana na shida zako, ishi nazo. Kila kitu kilichofanyika ulimwenguni kina suluhu na hakuna jambo geni. Ni vizuri kujua historia kwani kuna vile jambo linalofanyika kwa sasa lilisuluhishwa hapo awali. Soma ili uweze kujua namna shida zinatatuliwa” alisema Babu.

Mbunge huyo  hata hivyo alitaka serikali kuhalalisha bangi kwa madai kuwa inatumika kutibu magonjwa, kuongeza hamu ya chakula na kuongeza hamu ya mapenzi.

Ameitaka serikali kuhalalisha matumizi ya chang’aa, busaa na Muratina huku akisema kuwa ni pombe za kitamaduni na zinaongeza nguvu mwilini.

Ametaja uuzaji wa pombe za kitamaduni kama chan'gaa kuwa njia muhimu ya kupata mapato kwa watu wengi.

Amekiri kuwa wazazi wake waliuza Chang’aa akiwa mdogo ili kuweza kupata mapato ya kugharamia mahitaji ya pale nyumbani.

Hata hivyo, amesema kuwa unywaji wa pombe mingi waweza sababisha mvutano, kufanya tumbo kuwa kubwa na kuathiri utendaji wa tendo la ndoa.