DP Ruto:Tuko makini kuachana na siasa za mgawanyiko na kujenga nchi yenye umoja

Muhtasari
  • Naibu Rais William Ruto amesema uchaguzi mdogo katika kaunti ya Kiambu umeashiria kwamba Kenya haiitaji kubadilisha Katiba yake
  • Alisema nchi iko katika hatua ya kukomaa na hali ya kukosekana kwa utulivu wakati wa uchaguzi ilikuwa jambo la zamani
William Ruto
William Ruto
Image: Hisani

Naibu Rais William Ruto amesema uchaguzi mdogo katika kaunti ya Kiambu umeashiria kwamba Kenya haiitaji kubadilisha Katiba yake.

Alisema nchi iko katika hatua ya kukomaa na hali ya kukosekana kwa utulivu wakati wa uchaguzi ilikuwa jambo la zamani.

Akizungumza huko Mathioya, Murang’a Ijumaa, wakati wa mazishi ya Buku Munyori, baba wa mfanyikazi wake Munyori Buku, Ruto alisema shida pekee inayoikabili nchi ni viongozi ambao wanakataa kukubali matokeo ya uchaguzi.

"Tuko na nia ya kuachana na siasa za mgawanyiko na kujenga nchi yenye umoja. Kwa njia hiyo, tunaweza kusongesha nchi yetu mbele

Nafurahi sasa tunahamia kwenye siasa zinazohusu masuala ambayo tunaweza kuzungumza kama viongozi kwenye jukwaa la kubadilisha maisha ya Wakenya wa kawaida," Alizungumza DP Ruto.

Mbunge wa Kandara Alice Wahome aliwasifu watu wa Kiambu kwa kushiriki uchaguzi wa amani katika Jimbo la Kiambaa na Kata ya Muguga.

Mgombea wa chama cha United Democratic Alliance aliibuka mshindi  katika uchaguzi mdogo wa Kiambaa.

Njuguna Wanjiku alishinda dhidi ya mpinzani wake Kariri Njama wa Jubilee.

Kulingana na IEBC, Njuguna alipata kura 21,773 wakati mpinzani wake alifuatia kwa karibu na kura 21,263.

Hata hivyo, Joseph Githinji wa Chama cha Jubilee alishinda kiti cha Wadi ya Muguga, IEBC ilitangaza baada ya kujumlisha vituo vyote 29 vya kupigia kura.