Jamaa wawili washtakiwa kwa kujifanya waandishi wa habari ili waruhusiwe kuingia KICC

Muhtasari

•Mahakama iliwaachilia kwa dhamana ya Sh50,000 na kuagiza kesi hiyo itajwe tena mnamo Oktoba 8.

Image: THE STAR

Jamaa wawili walifikishwa mahakamani siku ya Ijumaa na kushtakiwa kwa kutoa maelezo ya uongo na kughushi kadi ya waandishi wa habari.

Fred Odanga na Thomas Ochieng walikanusha mashtaka matatu dhidi yao mbele ya hakimu David Ndungi.

Wawili hao wanatuhumiwa kuambia afisa wa uhusiano wa  umma katika idara  ya utumishi wa umma James Maina Macharia kwamba wao ni wanachama wa baraza la waandishi wa habari nchini mnamo Julai 9  ili waruhusiwe kuingia katika jengo la KICC.

Ilifumbuliwa kuwa wawili hao walikuwa wamedanganya.

Odanga alikabiliwa na mashtaka mengine ya kughushi ambapo inadaiwa alighushi kadi ya waandishi habari  akiwa mahali pasipojulikana jijini Nairobi akijifanya kuwa mwanachama wa MCK.

Washtakiwa waliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana wakidai kwamba wao ni waandishi mitandaoni ila si wanachama wa baraza la waandishi habari.

Mahakama iliwaachilia kwa dhamana ya Sh50,000 na kuagiza kesi hiyo itajwe tena mnamo Oktoba 8.