Wanafamilia 3 wafariki baada ya kuangukiwa na trela iliyobeba miwa Homa Bay

Muhtasari

•Victor Onjwayo, mke wake Caroline Akoth na mtoto wao mwenye umri wa miaka sita walikuwa wakisafiri kwa pikipiki kutoka soko la Rodi Kopany ajali ilipotokea.

•Msaidizi wa Chifu, Fredrick Onyango alisema trela hiyo ilipinduka baada ya kuondoka barabarani ili kuruhusu mabasi kupita.

Wakaazi wasimama karibu na eneo ambapo ajali ya barabarani ilitokea karibu na Rodi Kopany kando ya barabara ya Rodi-Ndhiwa mnamo Januari 18,
Wakaazi wasimama karibu na eneo ambapo ajali ya barabarani ilitokea karibu na Rodi Kopany kando ya barabara ya Rodi-Ndhiwa mnamo Januari 18,
Image: ROBERT OMOLLO

Mwanamume mmoja, mkewe na mtoto wao walifariki Jumatatu baada ya trela iliyokuwa ikisafirisha miwa kuwaangukia.

Victor Onjwayo, mke wake Caroline Akoth na mtoto wao mwenye umri wa miaka sita walikuwa wakisafiri kwa pikipiki kutoka soko la Rodi Kopany ajali ilipotokea.

Ajali hiyo ya saa mbili usiku ilitokea katika kijiji cha Wiobiero, karibu na soko la Rodi Kopany katika eneo bunge la Homa Bay Town.

Wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Daniel Ogeda walisema watatu hao walikuwa wamenaswa chini ya lundo la miwa.

"Hatukuweza kuondoa miwa haraka kwa kutumia mikono yetu. Kwa bahati mbaya, tuliwapata wakiwa wamefariki tulipowafikia,” Ogada alisema.

Msaidizi mkuu wa chifu katika eneo la Kalanya Kanyango, Fredrick Onyango alisema trela hiyo ilipinduka baada ya kuondoka barabarani ili kuruhusu mabasi kupita.

Dereva alishidwa kudhibiti trela hiyo na kuwaangukia Onjwayo na familia yake.

Onyango alisema miili hiyo ilitolewa baada ya wasimamizi wa kampuni ya Sukari Industries kuleta kreni ili kuinua trela.

Alisema trela ilianguka kutokana na uzito wa mzigo iliyokuwa imebeba.

"Barabara inafaa kupanuliwa kwa sababu ni nyembamba sana ili kuruhusu magari makubwa mawili kupita kwa wakati mmoja," Onyango alisema.

Miili hiyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Homa Bay Sammy Kosgey alisema vyombo vya usalama vinachunguza tukio hilo.

Alisema wanamtafuta dereva na kondakta wake ambao walitoroka baada ya ajali hiyo.

"Acha trela ziache kusafiri usiku kwa sababu baadhi yao hazina taa," Kosgey alisema.