Mwili wa mwanamke uliokuwa na maandishi 'Bwana ya mtu ni sumu' wapatikana umetupwa Ruiru

Muhtasari

•Maafisa walipata kijisanduku kilichokuwa na mwili wa mwanamke mwenye umri wa ujana kikiwa kimetupwa nje yaa kambi ya kikosi cha Recce iliyo Ruiru.

•Mikono na miguu ya mwanamke huyo ambaye bado hajatambulishwa ilikuwa imefungwa pamoja kwa kamba za manilla

Crime Scene

Hali ya mshtuko ilitanda katika eneo la Kimbo, kaunti ya Kiambu baada ya mwili wa binadamu kupatikana ukiwa umewekwa ndani ya kijisanduku Jumatatu jioni.

Ripoti ya polisi inasema kwamba maafisa walipata kijisanduku kilichokuwa na mwili wa mwanamke mwenye umri wa ujana kikiwa kimetupwa nje yaa kambi ya kikosi cha Recce iliyo Ruiru.

Inaripotiwa kwamba mwili huo ulikuwa umetiwa kwa gunia kisha kuwekwa ndani ya kijisanduku cheusi.

Mikono na miguu ya mwanamke huyo ambaye bado hajatambulishwa ilikuwa imefungwa pamoja kwa kamba za manilla. Ripoti ya polisi ilisema kwamba pia alikuwa amefungwa shingoni kwa kamba ya nailoni.

"Mwili huo ulikuwa na jeraha kubwa kwenye titi la kushoto. Alikuwa na maandishi ya wino kifuani, kwenye viganja vyote viwili vya mkono na mapaja yaliyosomeka "Bwana ya mtu ni sumu."," ripoti ya polisi ilisoma.

Wapelelezi kutoka Thika walikagua eneo la tukio kisha kupeleka mwili wa marehemu hadi City Mortuary huku uchunguzi wa maiti ukisubiriwa.