Polisi aliyesimamishwa kazi kwa kumpiga risasi mpenziwe apatikana akiwa amefariki mtoni, Meru

Muhtasari

•Afisa huyo alimpiga risasi mpenzi wake mara sita mnamo Agosti kufuatia baada ya kutofautiana nje ya Kituo cha Polisi cha Laare kisha akasimamishwa kazi.

•Polisi wanachunguza kubaini ikiwa ni afisa huyo alijitoa uhai ama aliuawa kisha mwili wake kutupwa mtoni.

Konstebo David Nyamweya ambaye mwili wake ulipatikana kwenye mto huko Meru mnamo Januari 15
Konstebo David Nyamweya ambaye mwili wake ulipatikana kwenye mto huko Meru mnamo Januari 15
Image: HANDOUT

Polisi katika kaunti ya Meru wanachunguza kisa ambapo afisa wa polisi aliyekuwa amesimamishwa kazi alipatikana.

Mwili wa Konstebo David Nyamweya, ambaye alikuwa anafanya kazi katika Kituo cha Polisi cha Mutuati, eneo la Igembe Kaskazini, ulipatikana ukielea katika Mto Kathita, karibu na mji wa Meru Jumamosi alasiri.

Afisa huyo alimpiga risasi mpenzi wake mara sita mnamo Agosti kufuatia baada ya kutofautiana nje ya Kituo cha Polisi cha Laare kisha akasimamishwa kazi.

Polisi walisema waliweza kumtambua  baada ya wachunguzi wa eneo la uhalifu kupata barua ya kusimamishwa kazi kutoka Januari 2, 2022, ndani ya mfuko wake.

Polisi wanachunguza kubaini ikiwa ni afisa huyo alijitoa uhai ama aliuawa kisha mwili wake kutupwa mtoni.

Kulingana na polisi, afisa huyo alipaswa kuhudhuria kikao cha polisi cha nidhamu mnamo Machi kwa matumizi mabaya ya bunduki kufuatia kitendo cha kutisha dhidi ya Everlyne Njoki mnamo Agosti 22, 2020 ambaye kwa bahati alinusurika kifo.

Kilichosababisha kifo cha afisa huyo bado hakijajulikana. Polisi wanashuku kiwewe kinachohusiana na kazi kama sababu ya kujitoa uhai pamoja na shambulio la hapo awali dhidi ya mpenziwe.

Mikakati ya kushughulikia hali ambayo imeona maafisa kadhaa wakifa katika visa kama hivyo inawekwa. Ni pamoja na kuundwa kwa kitengo cha ushauri nasaha ndani ya Tume ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi ili kuanzisha programu mbalimbali kuhusu suala hilo.

Mwili wa afisa huyo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.