Mwanamume afariki baada ya kuanguka kutoka ghorofa ya tatu Athi River

Muhtasari
  • Mwanamume afariki baada ya kuanguka kutoka ghorofa ya tatu Athi River
  • Joseph Mutisya alifariki papo hapo wakati wa tukio hilo la Ijumaa saa 10.00 asubuhi
Mwanamume afariki baada ya kuanguka kutoka ghorofa ya tatu Athi River
Image: George Owiti

Polisi huko Athi River wanachunguza kisa ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 43 alifariki baada ya kuanguka kutoka ghorofa ya tatu ya jengo huko Athi River, Kaunti ya Machakos.

Joseph Mutisya alifariki papo hapo wakati wa tukio hilo la Ijumaa saa 10.00 asubuhi.

Chifu msaidizi wa Athi River Martin Ngomo alisema mwanamume huyo aliteleza kutoka sakafuni alipokuwa akitengeneza dirisha kisa hicho kilipotokea.

Nyumba hiyo ni ya mwanasiasa mkuu katika Kaunti ya Machakos.

"Mwanamume huyo alikuwa akitengeneza kioo cha dirisha kwenye nyumba ambayo iko karibu na Champions of Christ International Church huko Athi River, alifariki papo hapo," Ngomo alisema.

Afisa wa upelelezi wa DCI katika uchunguzi alisema mwili huo ulipelekwa hadi chumba cha kuhifadhi maiti cha Machakos.

Mwili wa mwanamume huyo ulitolewa katika eneo la tukio na maafisa wa kituo cha polisi cha Athi River.

Wakazi walilaani kisa hicho wakisema kuwa nyumba ambayo ilis ababisha kifo cha mwanamume huyo ilikuwa katika hali duni.

"Tunashangaa kwa nini jengo hili halijalaaniwa na mamlaka husika za serikali. Mtu huyu angekuwa hai kama nyumba hiyo ingekuwa katika hali nzuri," shahidi aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuhofia kushtakiwa aliambia Star.

Ngomo alisema mtu huyo alianguka chini kutoka nje ya jengo hilo.

Alisema wananchi wanapaswa kuacha porojo juu ya tukio hilo na badala yake waache mamlaka husika kufanya uchunguzi wao.