'Ulipumua ya mwisho nikiwa nimekushika mkono,' Rigathi amkumbuka marehemu kakake kwa ujumbe wa kihisia

Muhtasari

•Nderitu ambaye alikuwa gavana wa kwanza wa Nyeri alifariki mnamo Februari 24, 2017  kutokana na saratani ya kongosho.

•Rigathi amemtaja marehemu ndugu yake kama mshauri wake wa siasa huku akisema anapeza mawaidha na mchango wake katika siasa za kitaifa.

Marehemu Rigathi Gachagua
Marehemu Rigathi Gachagua
Image: FACEBOOK// RIGATHI GACHAGUA

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua angali anamuomboleza  marehemu ndugu yake Nderitu Gachagua  miaka mitano miaka mitano baada ya kufariki kwake.

Mwandani huyo wa naibu rais William Ruto ameadhimisha nusu mwongo tangu kufariki kwa Nderitu kwa chapisho la kihisia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

"Asubuhi moja mapema miaka mitano iliyopita katika baridi kali ya London ulikata pumzi yako ya mwisho nikiwa nimekushika mkono. Uso wako uliojaa ujasiri na dhamira, baada ya mapambano ya miaka mitatu na saratani ya kongosho, ulikubali kwa neema kwamba safari ilikuwa imekamilika" Rigathi aliandika.

Nderitu ambaye alikuwa gavana wa kwanza wa kaunti ya Nyeri alifariki mnamo Februari 24, 2017  kutokana na saratani ya kongosho.

Rigathi amesema maisha yake pamoja na wanafamilia wengine haijawahi kuwa sawa tena tangu kufariki kwa mwanasiasa huyo wa zamani.

Amesema wanafamilia wanapeza jinsi mbunge huyo wa zamani wa Mathira aliweka familia yao pamoja na kuwaongoza kwa upendo, ukarimu na busara nyingi.

"Tunapeza upendo wako, huruma, ukarimu na uongozi uliotoa kwa familia yetu kwa kujitolea. Karamu za Krismasi ulizotuandalia Pwani hazipo tena. Mikutano ya famila ambayo uliendelea kusisitiza ifanyike ilififia baada ya kuondoka kwako. Nafasi yako katika familia inabaki tupu na wengi wetu tunabaki kukana kwamba hautarudi tena" Aliandika.

Rigathi amemtaja marehemu ndugu yake kama mshauri wake wa siasa huku akisema anapeza mawaidha na mchango wake katika siasa za kitaifa.

"Tunaishi katika nyakati zisizo na kifani za udikteta na mateso. Laiti ungekuwa hapa kaka, nina hakika ungeniongoza jinsi ya kushughulikia usaliti wa mtu niliyemtumikia kwa uaminifu kwa miaka ishirini. Nimejaribu kuwa jasiri kwa njia ambayo ungekubali lakini sio rahisi. Familia yetu inaogopa sana na sasa wanazungumza kwa sauti ya chini. Wanaishi kwa hofu na mashaka bila kujua kesho itakuwaje" Amesema.

Mbunge huyo amemtakia marehemu nduguye mapumziko ya amani huku akimhakikishia upendo mkubwa kwake ambao unaishi ndani yake.