'Wanawake wako salama mikononi mwa nani?' Milly Wajesus, Betty Kyalo, Size 8 walaani tukio la Forest Road

Muhtasari

•Tukio hilo lilitokea katika barabara ya Forest Road, jijini Nairobi. Kufikia sasa takriban washukiwa 16 wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

•Hakimu Mkuu Martha Koome alitoa taarifa kuhusiana na tukio hilo na kutaka wahusika wote kutiwa mbaroni na kushtakiwa

Mwanamke ashambuliwa na wanaboda katika barabara ya Forest Road
Mwanamke ashambuliwa na wanaboda katika barabara ya Forest Road
Image: KWA HISANI

Mada ambayo imekuwa ikiangaziwa zaidi mitandaoni katika kipindi cha siku moja ambacho kimepita ni kuhusu tukio ambapo kikundi cha waendesha bodaboda kinaripotiwa kushambulia dereva  mwanamke baada ya kuhusika kwenye ajali na mmoja wao.

Katika kanda ya video ambayo imesambazwa mitandaoni, mwanamke mwenye umri wa ujana anaonekana akinyanyaswa kingono na kikundi kikubwa cha wanaume wanaominika kuwa waendesha pikipiki.

Tukio hilo lilitokea katika barabara ya Forest Road, jijini Nairobi. Kufikia sasa takriban washukiwa 16 wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Maelfu ya Wakenya wakiwemo maafisa wa serikali, wasanii na watu mashuhuri wameendelea kukashifu tukio hilo la kuchukiza.

Mwanavlogu Millicent Wambui (Milly Wajesus), mtangazaji Betty Kyalo, mwanamuziki Linet Munyasi (Size 8) na Hakimu Mkuu Martha Koome ni baadhi ya watu ambao wamejitokeza kutetea usalama na heshima kwa wanawake wenzao.

"Nimetazama kwa masikitiko video hiyo mbaya ya mwanadada akinyanyaswa katika barabara ya Forest Road. Ni jambo la kuvunja moyo tu. 💔💔Inakuwaje wanaume hao wote wamgeukie mwanamke mmoja. Tabia gani hiyo ya kinyama kwa mwanadamu aliye hatarini na asiye na uwezo wa kusababisha madhara.Ni aibu kwao  pamoja na wote waliosimama kutazama tukio hilo la kutisha bila kufanya chochote. Je, hawa wanaume hao wasio na aibu hawana dada, mama au binti. Jamii hii inapaswa kuwaheshimu na kuwalinda wanawake kwa ukatili. Hilo ni la kutisha tu. Natumai atakuwa sawa," Betty Kyalo alisema.

Milly Wajesus alitaja tukio hilo kuwa la kinyama huku akiomba haki ipatikane na  adhabu kali ichukuliwe dhidi ya wahusika.

"Je, watu wanawezaje kukosa ubinadamu? Mikononi mwa nani wanawake wako salama? Inatia kiwewe sana! Namhurumia msichana huyo, Haki inahitaji kupatikana! Aibu kwa wanaumehao  washenzi. Ni furaha kuona wanawindwa," Milly alisema.

Size 8 alisema kuwa hata alishindwa kutazama video hiyo kwa kuwezwa na hisia. Aliwataka wanaboda wakomeshwe dhidi ya tabia kama iliyoshuhudiwa kwenye video hiyo.

Hakimu Mkuu Martha Koome alitoa taarifa kuhusiana na tukio hilo na kutaka wahusika wote kutiwa mbaroni na kushtakiwa.Koome alitaka haki za Wakenya wote  na usalama wao kulindwa siku zote.

"Ninakashifu kitendo hiki kama cha kinyama na kinachohitaji uangalizi wa juu zaidi wa kisheria. Wanawake wa Kenya, wasichana na raia lazima walindwe na wajisikie salama katika nchi yao. Hiki ni kipaumbele ambacho lazima tuendelee kukifuata. Kila shirika linajitolea kwa upande wake kukomesha unyanyasaji wa kijinsia na kijinsia," Koome alisema.

Wakenya wengine wengi wameendelea kutoa hisia zao kuhusiana na tukio hilo huku wengi wakiashiria kero kubwa.