Arati asema maisha yake yamo hatarini, aandikisha taarifa DCI

Mawakili wa Simba Arati anadai kuwa njama hiyo inahusisha kupekua nyumba zake Kisii na Nairobi kwa madai ya kumiliki bunduki kinyume cha sheria.

Muhtasari
  • Aliongeza: "Kwa sehemu hii ni kuhakikisha kuwa Gavana Arati hapewi nafasi ya kutekeleza majukumu yake kama Gavana wa Kisii."
Gavana wa kaunti ya Kisii
Gavana wa kaunti ya Kisii
Image: Facebook

Gavana wa Kisii Simba Arati anataka uchunguzi ufanywe kuhusu kile anachodai njama ya idara ya DCI katika Kaunti ya Kisii kumkamata na baadhi ya wafuasi wake.

Arati, ambaye alirekodi taarifa katika makao makuu ya DCI jijini Nairobi akiwa na mawakili wake Gavana James Orengo na Otiende Amolo, anadai kuwa njama hiyo inahusisha kupekua nyumba zake Kisii na Nairobi kwa madai ya kumiliki bunduki kinyume cha sheria.

Akihutubia wanahabari siku ya Jumatatu, Orengo alisema wamewasilisha kwa makao makuu ya DCI rekodi ya sauti iliyonasa Afisa wa Upelelezi wa Jinai (CCIO) katika Kaunti ya Kisii akidaiwa kuzungumza kuhusu njama ya kutega bunduki nyumbani kwa Arati.

"Tumewapa polisi nakala ya klipu hiyo ambapo CCIO huko Kisii amerekodiwa akitoa maagizo na maarifa kuhusu jinsi bunduki na vitu vingine vitawekwa kwa gavana Arati," Orengo alisema.

Aliongeza: "Kwa sehemu hii ni kuhakikisha kuwa Gavana Arati hapewi nafasi ya kutekeleza majukumu yake kama Gavana wa Kisii."

Kwa upande wake, wakili mkuu Otiende Amolo alisema DCI iliahidi kushughulikia suala hilo.

“Ni malalamiko ya kipekee. Gavana Arati amewasilisha malalamishi kwa DCI dhidi ya DCI. Wametuhakikishia kuwa hatua zitachukuliwa hivyo tusubiri tuone hatua hiyo kwa sababu mbadala wake ni kujichukulia sheria mkononi,” alisema.