Watu 6 wafariki katika ajali kwenye barabara ya Narok-Mulot

Ajali hiyo ilitokea karibu na eneo la Silanga takriban kilomita nne kutoka mji wa Narok.

Muhtasari
  • Momanyi alisema kuwa ajali hiyo ilitokea wakati  gari aina ya Toyota Sienta ilipogongana uso kwa uso na gari aina ya Subaru Forester.
  • Waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali tofauti mjini Narok.
Ajali
Ajali
Image: HISANI

Takriban watu sita wamethibitishwa kufariki na wengine saba kujeruhiwa katika ajali ya barabarani kwenye barabara ya Narok-Mulot.

Ajali hiyo ilitokea karibu na eneo la Silanga takriban kilomita nne kutoka mji wa Narok.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Narok ya Kati John Momanyi alisema kuwa ajali hiyo ilitokea wakati  gari aina ya Toyota Sienta ilipogongana uso kwa uso na gari aina ya Subaru Forester.

"Dereva wa Subaru Forester alikuwa akijaribu kulipita gari lingine na kugongana uso kwa uso na Subaru iliyokuwa ikisafiri upande wa pili," alisema Momanyi.

Subaru Forester ilikuwa ikielekea Narok kutoka Bomet huku dereva wa Toyota Sienta akielekea upande wa Mulot.

Momanyi alisema kuwa watu hao sita akiwemo dereva wa Toyota Sienta walifariki papo hapo

Waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali tofauti mjini Narok.

Dereva wa Subaru Forester alilalamikia maumivu ya kifua na kukimbizwa katika Hospitali ya Cottage.

Magari yote mawili yalivutwa hadi katika yadi ya Kituo cha Polisi cha Narok yakisubiri kukaguliwa.

Hii ni ajali mbaya ya hivi punde zaidi kutokea huku kukiwa na kampeni kali ya kukabiliana na tishio hilo.

Zaidi ya watu 1,000 wamefariki katika muda wa miezi mitatu iliyopita katika ajali tofauti.

Wengine wengi wanauguza majeraha kufuatia ajali hizo.