KRA yataka CCTV kuwekwa kwenye viwanda vya pombe

Muhtasari
  •  Kamera za CCTV pia zitamruhusu mtoaji ushuru kufuatilia kile ambacho makampuni yanazalisha, kwa kupeleka data katika muda halisi.
Kamishna jenerali wa KRA, Githii Mburu
Kamishna jenerali wa KRA, Githii Mburu
Image: Maktaba

Hivi karibuni, huenda mbio za sakafuni za wagema mivinyo kuishia ukingoni baada ya mamlaka ya kutoza ushuru ya KRA kutangaza kwamba itawataka wagemaji wote kuweka kamera za siri almaarufu CCTV ili kufuatilia shughuli zote za ugemaji kama mbinu moja ya kuwanasa wagemaji haramu na pia kuimarisha shughuli ya utozaji ushuru.

Kulingana na gazeti moja la biashara nchini, KRA inawataka watengenezaji wa pombe wote pia kando na kuweka CCTV, pia wanatakiwa kuweka mita za upitishaji umeme katika viwanda vyao vya vileo kama hatua moja ya kuzuia ukwepaji wa kodi na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ushuru.

Kamera za CCTV pia zitamruhusu mtoaji ushuru kufuatilia kile ambacho makampuni yanazalisha, kwa kupeleka data katika muda halisi.

Gazeti hilo linaripoti kwamba hii si mara ya kwanza kwa mita hiyo kutakiwa kuweka kwenye viwanda hivyo kwani mwaka wa 2011 kilitekelezwa kwa vileo vikali kama whisky, brandy, na gin, lakini sasa kinatazamiwa kutambulishwa kwa tasnia nzima ya vileo ikijumuisha bia na taratibu kwa bidhaa zingine zinazotozwa ushuru kama vile maji.

“Mwaka huu, tumekuja na njia kali sana ya kuhakikisha watengenezaji wote wa pombe wanawekewa vifaa vitatu muhimu ikiwa ni pamoja na, flow meter ya molekuli, rada ya kufuatilia kinachoingia kwenye matangi yao, na kamera za CCTV. Vifaa hivi vyote vitaunganishwa na kuhakikisha kuwa vinaweza kutuma data kwa mbali,’’ alisema Isaac Gachoka, afisa wa usimamizi wa ushuru wa ndani wa Mamlaka ya Ushuru wa Kenya (KRA).

 

Hatua ya hivi punde inajiri huku kukiwa na mzozo kati ya mamlaka ya kutoza ushuru ya KRA na Keroche Breweries ambapo kampuni hiyo inalaumiwa kwa kukosa kulipa Shilingi bilioni 22.79 za ushuru kwa miaka 16.Je, unahisi sheria hii mpya kutoka kwa KRA ni njia mojawapo ya kuimarisha uzalishaji wa vileo vyenye haiba iliyotukuka nchini ama ni mbinu ya kukandamiza sekta ya vileo?