Raila amteua Tuju kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Azimio

Muhtasari

•Tuju tayari amekubali kuchukua nafasi hiyo ya uongozi aliyokabidhiwa na ataanza kazi mara moja.

Aliyekuwa Katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju
Aliyekuwa Katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju
Image: MAKTABA

Aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha Jubilee, Raphael Tuju ameteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa sekretarieti ya muungano wa Azimio la Umoja.

Tuju ambaye alijiuzulu Jubilee mwezi Machi amepatiwa wadhfa huo mpya na kinara wa ODM Raila Odinga ambaye ndiye mpeperusha bendera wa Azimio katika uchaguzi wa urais wa mwaka huu.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, Tuju tayari amekubali kuchukua nafasi ya uongozi aliyokabidhiwa na ataanza kazi mara moja.

"Tuju ataratibu vyama vyote vya Azimio na ataongoza timu za mikakati na programu zitakazofanya kazi kuhakikisha Azimio inashinda katika uchaguzi wa Agosti," Taarifa iliyotiwa saini na msemaji wa ODM Dennis Onyango ilisoma.

Muungano wa Azimio unajumuisha zaidi ya vyama 20 vikiwemo Jubilee, ODM, Wiper, NARC-K na vinginevyo.

Tuju alijiuzulu kama kama katibu mkuu wa Jubilee takriban miezi miwili iliyopita baada ya kuhudumu kwa miaka tisa.