Rais Kenyatta atangaza tarehe ya kufanyika vikao vya kwanza vya bunge

Haya yanajiri siku chache baada ya viongozi wa Kenya Kwanza kuteta kucheleweshwa kwa tangazo hilo.

Muhtasari

• Rais ametoa tangazo hilo Jumatatu huku taifa likifuatilia uamuzi wa mahakama ya upeo kuhusu kesi inayopinga kuchaguliwa kwa Ruto kama rais wa 5.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru ametangaza kikao cha kwanza cha wabunge na maseneta wapya waliochaguliwa kufanyika Alhamisi, Septemba 8.

Katika chapisho la gazeti la serikali siku ya Jumatatu, Septemba 5, wabunge na maseneta wataapishwa na kisha kuchagua maspika.

“Katika kutekeleza mamlaka yaliyotolewa na Ibara ya 126 (2) ya Katiba ya Kenya, I. Uhuru Kenyatta, Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, natangaza kuwa Mkutano wa Kwanza wa Bunge na Seneti utafanyika katika Majengo ya Bunge Kuu katika Ukumbi wa Seneti, Nairobi, Septemba 8, 2022, saa 9.00 asubuhi," ilisema taarifa hiyo kwa sehemu.

Kulingana na wajuzi wa katiba, Kifungu cha 126(2) cha Katiba, kilimtaka Uhuru kuchapisha muda na eneo la bunge la kwanza lililoketi ndani ya siku 30.

Raia anayeondoka Kenyatta amefanya tangazo hilo siku chache baada ya baadhi ya viongozi kutoka kwa mrengo wa Kenya Kwanza kuteka kwamba alikuwa anafanya makusudi kuchelewesha kwa kufanya tangazo hilo licha ya viongozi hao wote kuchaguliwa na kukabidhiwa vyeti vya ushindi.

Siku hiyo, viongozi hao teule watatarajiwa kufanya kikao cha kwanza ambacho kitakuwa ni kuwachagua maspika katika majumba yote mawili; bunge la kitaifa na lile la seneti.

Muungano wa Kenya Kwanza tayari umewasilisha jina la seneta wa Bungoma Moses Wetangula kuwa spika wa bunge la Kitaifa.

Wetangula anatarajiwa kuachia kazi kama seneta, nafasi ambaye ameitetea kwa mara ya tatu mtawalia na atamenyana na spika wa zamani Kenneth Marende wa muungano wa Azimio ambaye pia anataka kurejea kama spika.