Huru tena! Fahamu maagizo aliyopewa mchungaji Ezekiel baada ya kuachiliwa

Odero alikamatwa wiki jana kwa kuhusishwa pakubwa na mauaji ya kimbari katika shamba la Mackenzie huko Shakahola.

Muhtasari

• Mchungaji Ezekiel pia alizuiwa kutoa maoni hadharani kuhusu Mauaji ya Shakahola huku uchunguzi ukiendelea.

• Mahakama pia ilimwamuru kuripoti kwa DCI mara moja kwa wiki.

Pasta Ezekiel akamatwa, mbunge wa Magarini amtetea vikali.
Pasta Ezekiel akamatwa, mbunge wa Magarini amtetea vikali.
Image: Twitter

Mchungai mwenye utata Ezekiel Odero wa kanisa la New Life huko Mavueni kaunti ya Kilifi hatimaye ameachiliwa huru kwa dhamana ya pesa taslimu shilingi milioni moja na mahakama ya Shanzu Alhamisi alasiri.

Mchungaji huyo alitakiwa kulipa kiasi hicho au kutoa bondi mbadala ya shilingi milioni 3 huku uchunguzi dhidi ya kanisa lake ukiendelea.

Mchungaji Ezekiel pia alizuiwa kutoa maoni hadharani kuhusu Mauaji ya Shakahola huku uchunguzi ukiendelea.

Mahakama pia ilimwamuru kuripoti kwa DCI mara moja kwa wiki.

"Wahusika watakuwa na uhuru wa kutuma maombi ya kufungwa kwa faili hii uchunguzi utakapokamilika," hakimu katika Mahakama ya Shanzu.

Mawakili wake, Cliff Ombeta na Danstan Omari, walikuwa wameomba mahakama kutupilia mbali ombi la polisi wakitaka kumzuilia kwa siku 30 zaidi.

Polisi walikuwa wametoa ombi la kumshikilia Odero kwa siku 30 zaidi, jambo ambalo mawakili hao wake walilipinga vikali huku wakiitaka mahakama kumuachilia huru kwa dhamana kama moja ya takwa la kikatiba.

Mnamo Mei 2, Mahakama ilitoa uamuzi wa kumshikilia Odero kwa siku mbili Zaidi hadi Alhamisi Mei 4 ambapo kesi yake ilirejelewa kutathmini iwapo angeachiliwa.

Mchungaji huyo alitiwa nguvuni wiki jana na makachero wa DCI huko Kilifi na waziri wa usalama wa ndani Kindiki alitoa agizo la kufungwa mara moja kwa kanisa lake huko Mavueni.

Ezekiel anahusishwa pakubwa na uchunguzi wa mauaji ya kimbari huko Shakahola katika shamba la mchungaji mwingine mwenye itikadi potovu Paul Mackenzie ambapo inadaiwa Ezekiel alikuwa anasafirisha miili ya watu waliokuwa wanafariki Mavueni kwenda kuzikwa Shakahola.

Pia inadaiwa kwamab wawili hao wanashirikiana katika biashara na Mackenzie aliwahi kumuuzia Odero kituo cha runinga.

 Licha ya kanisa lake kufungwa, waumini wa Odero wamekuwa wakikita kambi nje ya kanisa hilo lakini pia nje ya mahakama wakiimba na kusujudu huku wakiitaka mahakama kumuachilia huru mchungaji wao kwa kile wanahisi kwamba anawindwa bila hatia.