Tetemeko kubwa la ardhi laua takriban watu 304 na kujeruhi zaidi ya 1,800 Haiti

Haiti bado inajikwamua kutoka kwa athari za tetemeko baya la ardhi la mwaka 2010.

Muhtasari

•Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.2 katika vipimo vya Ritcher - liligonga magharibi mwa nchi hiyo Jumamosi asubuhi, kuvunja na kuharibu majengo ikiwemo makanisa na hoteli.

•Mwaka 2010 tetemeko la ardhi lilokumba Haiti liliwaua watu zaidi ya 200,000 na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu na uchumi.

Karibu watu 304 wamefariki na wengine wengi kujeruhiwa
Karibu watu 304 wamefariki na wengine wengi kujeruhiwa
Image: GES

Tetemeko kubwa la ardhi limekumba Haiti, kuua karibu watu 304 na kuwajeruhi zaidi ya 1,800.

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.2 katika vipimo vya Ritcher - liligonga magharibi mwa nchi hiyo Jumamosi asubuhi, kuvunja na kuharibu majengo ikiwemo makanisa na hoteli.

Waziri mkuu amesema ulikuwa "uharibifu mkubwa " na kutangaza mwezi mmoja wa hali ya hatari.

Haiti bado inajikwamua kutoka kwa athari za tetemeko baya la ardhi la mwaka 2010.

Kina cha tetemeko hilo la Jumamosi kilikuwa karibu kilo mita 12 ( maili 7.5) kutoka mji wa Saint-Louis du Sud, uchunguzi wa wanajiolojia wa Marekani (USGS) umesema.

Mtetemeko huo ulisikika katika mji mkuu wa Port-au-Prince uliyo na wakazimwengi, umbali wa kilomita 125, na mataifa jirani.

"Nyumba nyingi ziliharibiwa, watu wamefariki na wengine wako hospitali," Christella Saint Hilaire, ambaye anaishi karibu na kina cha tetemeko hilo, aliiambia shirika la habari la AFP.

Waiziri Mkuu Ariel Henry alisema ameandaa timu ya kufanya kazi ya kutoa misaada.

"Kitu cha muhimu ni kuokoa manusura wengi iwezekanavyo waliokwama kwenye vifusi," alisema. "Tumefahamishwa kuwa hospitali zimelemewa na kazi hasa ile ya Les Cayes inayowahudumia wale waliojeruhiwa na watu waliovunjika."

Baadaye Bw Henry alifichua kwamba alisafiri kwa ndege juu ya mji wa Cayes.

Rais Joe Biden ameamuru Marekani ''kuingilia kati mara moja" kusaidia nchi hiyo na kusema kwamba shirika la USAID litasaidia katika juhudi za "kutathmini uharibifu na kuwaokoa wale waliojeruhiwa na wale ambao watalazimika kujenga tena".

"Katika kile ambacho ni wakati mgumu kwa watu wa Haiti, Nimefadhaishwa na tetemeko hili," alisema.

USGS awali ilionya kuwa tetemeko hilo huenda likasababisha maelfu ya vifo na majeruhi. Pia limesema kuwa mitetemeko mengine sita ilisikika katika maeneo hayo ikiwemo moja lenye ukubwa wa 5.1.

Watu wakitembea katika mtaa uliofurika maji mjini Les Cayes
Watu wakitembea katika mtaa uliofurika maji mjini Les Cayes
Image: EPA

Frantz Duval, mhariri wa mkuu wa gazeti la Le Nouvelliste nchini Haiti, aliandika kwenye Twitter kuwa hoteli mbili ni miongoni mwa majengo yaliyoharibiwa katika mji wa Les Cayes. Alisema hospitali katika eneo hilo zimelemewa na kazi.

Waandishi wa habari huko Le Nouvelliste baadaye walisema makanisa mengi na hoteli katika pwani ya kusini zimeporomoka au kuharibiwa vibaya.

Archdeacon Abiade Lozama, mkuu wa kanisa la Episcopal mjini Les Cayes, aliiambia gazeti la New York Times: "Barabara zilijaa kelele, Watu walikuwa wakiwatafuta wapendwa wao, mali zao au huduma ya afya na maji."

Watu wakitembea katika mtaa uliofurika maji mjini Les Cayes
Watu wakitembea katika mtaa uliofurika maji mjini Les Cayes
Image: EPA

Picha zilizowekwa katika mitandao ya kijamii zinaonesha majengo yaliyoporomoka na mkusanyiko wa vifusi baada ya tetemeko hilo.

Leila Bourahla, Mkurugezi wa shirika la Haiti la Save the Children, ameliambia gazeti la New York Times kwamba itachukua siku kadhaa kutathmini uharibifu lakini "ni wazi kuwa hili ni janga kubwa la kibinadamu"

Naomi Verneus, 34- mkazi wa jiji kuu la Port-au-Prince, aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba aliamshwa na mtetemeko huo na kitanda chake kilikuwa kikitikisika.

"Nilipoamka sikuwa hat ana muda wa kuvaa viatu. Tuliponea tetemeko la ardhi la mwaka 2010 kwa hivyo kilichonijia akilini ni kukimbia. Baadae nilikumbuka watoto wangu wawili na mama yangu mzazi walikuwa ndani ya nyumba. Majirani zangu walienda kuwaambia watoke nje. Tulikimbia barabarani," alisema.

Mwaka 2010 tetemeko la ardhi lilokumba Haiti liliwaua watu zaidi ya 200,000 na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu na uchumi.

Tetemeko la Jumamosi limetokea kukiwa na mzozo wa kisiasa nchini, kufuatia kuawa kwa rais mwezi uliopita.

Nyota wa mchezo wa Tennis Naomi Osaka, ambaye ana kizazi cha Japan na Haiti, ameweka ujumbe Twitter kusimama na Haiti.

Akiangazia mashinano ya wiki ijayo ya Western & Southern Open, mshindi huyo mara nne wa Grand Slam aliandika: "Nakaribia kushiriki mashindano wiki hii, nitatumia pesa ushindi kusaidia katika juhudi za msaada kwa Haiti. Najua 'damu ya mababu zetu ina nguvu tutaendelea kuongezeka."