Polisi wa DR Congo ahukumiwa kifo kwa mauaji ya mwanaharakati

Muhtasari
  • Polisi mwingine, Jacques Migabo, pia alihukumiwa kifungo cha miaka 12 wakati wa kesi hiyo
Image: AFP

Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imemhukumu kifo polisi wa ngazi ya juu kwa kuhusika katika mauaji ya mwanaharakati wa haki za binadamu Floribet Chebeya mwaka wa 2010, ambayo yalisababisha ghadhabu ya kitaifa.

Kamishna wa polisi Christian Ngoy Kenga alipatikana na hatia ya mauaji, kukimbia na matumizi mabaya ya silaha. Mwili wa Bw Chebeya ulipatikana ukiwa umefungwa kwenye gari lake mjini Kinshasa.

Kuna kusitishwa kwa adhabu za kifo nchini DR Congo. Hata hivyo, hukumu ya kifo haijafutwa na mahakama za kijeshi zinaendelea kutoa hukumu hizo.

Polisi mwingine, Jacques Migabo, pia alihukumiwa kifungo cha miaka 12 wakati wa kesi hiyo.

Alikiri kuwanyonga Bw Chebeya na dereva wake, Fidèle Bazana. Kamishna wa polisi Paul Mwilambwe, ambaye alikuwa shahidi mkuu katika kesi hiyo, aliachiliwa, Radio Okapi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa imesema.

Bw Mwilambwe, ambaye alitoroka tangu mauaji hayo na kurejeshwa nyumbani mwaka jana, alimtaja Rais wa zamani Joseph Kabila na mkuu wa zamani wa polisi Jenerali John Numbi, kuwa waliamuru mauaji hayo.

Si Bw Kabila wala Jenerali Numbi ambaye ametoa maoni yao hadharani, lakini mahakama ya kijeshi imemshtaki jenerali huyo kwa mauaji ya Bw Chebeya na dereva wake.

 

 

Polisi ahukumiwa kifo kwa mauaji ya mwanaharakati