Serikali yashtushwa na taarifa ya watoto kufundishwa kulawitiana shuleni - Tanzania

Waziri wa Elimu wa Tanzania amesema kuwa taarifa ambazo zimetoka kwenye baadhi ya vyombo vya habari

Muhtasari

• Mwanzoni mwa juma kuliripotiwa kuhusu uwepo wa matukio ya kufundisha watoto kulawitiana katika baadhi ya shule zilizopo mkoani Kilimanjaro.

Image: Getty Images

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa taarifa ambazo zimetoka kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuhusu shule ambazo watoto wamekuwa wakifundishwa vitendo vya kulawitiana zimewashtua.

Amesema kuwa sasa hivi wanapitia hizo shule zilizotajwa na kujaribu kupata ukweli kuhusu jambo hili.

‘’Tumelichukua kwa umuhimu mkubwa sana, tumeshtushwa sana na taarifa hizo, tumepeleka Kamishna wa elimu, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora pamoja na mwanasheria wa wizara waende haraka’’.

‘’Tumeongea na Mkuu wa Mkoa kumuomba asaidiane na timu iliyokwenda kule pamoja na kutusaidia ili sehemu iliyo na masuala ya jinai, polisi wachukue hatua mara moja’’.

Bw. Mkenda amesema kwasababu suala hilo limetokea katika eneo moja, kunaweza kukawa na taarifa katika maeneo mengine hivyo Katibu Mkuu wa Wizara atatangaza namba ambayo itawezesha watu kutoa taarifa iwapo mtu yoyote akijua kuna vitendo kama hivyo katika shule yoyote hapa Tanzania, ya Umma au binafsi au vyuoni, anaweza akapiga simu akatoa taarifa na mamlaka itafuatilia.

‘’Tunaongeza umakini wa kufuatilia mambo haya kwasababu tunajua yanaweza kuchafua taswira ya elimu, yanaharibu vijana wetu, yatasababisha wazazi wakose imani na shule, sisi tutaendelea kufanya uchunguzi na kudhibiti jambo hilo.’’ Alisema Prof. Mkenda

Mwanzoni mwa juma kuliripotiwa kuhusu uwepo wa matukio ya kufundisha watoto kulawitiana katika baadhi ya shule zilizopo mkoani Kilimanjaro.