Raia wa TZ aliyefariki vitani Urusi aagwa bila jeneza kufunguliwa

Nemes Tarimo alikwenda Urusi kwa ajili ya masomo lakini katikati akajiunga na kundi la wapiganaji la Wagner ili kupambana na Ukraine.

Muhtasari

• Baada ya kufungwa miaka 7, alitakiwa kununua uhuru wake kwa kujiunga vitani kama kupata dhamana.

Nemes Tarimo aagwa bila kufunguliwa jeneza
Nemes Tarimo aagwa bila kufunguliwa jeneza
Image: Ayo TV

Nemes Tarimo, raia wa Tanzania aliyefia vitani nchini Urusi aliagwa jana nyumbani kwao baada ya kupokelewa kutoka Urusi mapema siku hiyo.

Kulingana na taarifa zilizkuwemo, Tarimo alikwenda Urusi miaka kadhaa iliyopita kwa ajili ya masomo lakini akafanya kosa ambalo halikutajwa kumpelekea kufungwa miaka saba jela.

Baada ya kuzuka kwa vita kati ya Ukraine na Urusi, rais huyo aliyekuwa jela kuhudumia kifungo chake alitakiwa kuchagua moja kati ya kutumikia kifungo chake jela au kununua uhuru wake kwa kujiunga katika kundi binafsi ya upiganaji la Wagner ili kushiriki vita dhidi ya Ukraine.

Maskini wa Mungu alichagua kujiunga vitani ili itakapomalizika aachiliwe huru kabisa, lakini hili halikutokea kwani uhai wake ulikatishwa ghafla akiwa vitani na kundi la Wagner la nchini Urusi.

Baada ya mwili wao kupokelewa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, ulisafirishwa moja kwa moja hadi nyumbani kwao Mbeya kwa ajili ya maziko.

Kilichoshangaza wengi, jeneza lake halikupata kufunuliwa ili watu wadhibitishe kama kweli ni yeye au walikabidhiwa mwili ghushi wa mtu asiye wa kwao.

Familia ilisema kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao jeneza halitofunguliwa hivyo Ndugu, Jamaa na Marafiki waliaga picha na jeneza.

“Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu tutatumia mtindo wa kuaga sanduku pamoja na picha hatutaweza kulifungua sanduku kwasababu zilizo nje ya uwezo wetu,” mmoja wa wanafamilia aliarifu Ayo TV.

Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya Tanzania iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki mapema wiki hii, Nemes alifariki akiwa vitani nchini Ukraine baada ya kujiunga na Jeshi binafsi la Urusi la Wagner Group akiwa anatumikia sehemu ya kifungo chake cha miaka saba alichofungwa kwa makosa ya kihalifu.

Waziri Tax alinukuliwa akisema "Tarimo akiwa gerezani alipewa nafasi ya kujiunga na kikundi cha kijeshi cha Wagner kwa ahadi ya kulipwa fedha lakini kwa ahadi ya kuachiwa huru mara baada ya vita na umauti ulimkuta October 24,2022 na Wizara ikawasiliana na Serikali ya Urusi ili kukabidhiwa mwili"

“Nemes Tarimo alikwenda nchini Urusi mwaka 2020 kwa masomo ya shahada ya uzamili katika fani ya biashara, March 2022 alihukumiwa kifungo cha miaka saba kwa vitendo vya uhalifu,” Ayo TV waliripoti.