Mamilioni ya watu wahudhuria ibada ya Pope Francis, Kinshasa

Ziara ya awali ya Papa ilibidi iahirishwe kwa sababu ya afya yake.

Muhtasari

• Siku ya pili ya ziara yake inaenda sambamba na mwendelezo wa mapigano kati ya jeshi la Kongo na waasi.

Image: AFP

Papa Francis ameadhimisha ibada kubwa mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Ni zaidi ya miaka 37 tangu papa kufanya ziara katika taifa hilo lenye utajiri wa madini lakini ikiwa nchi inayokabiliwa na migogoro.

Inakadiriwa kuwa watu wapatao milioni walikusanyika katika eneo la wazi kwa ajili ya ibada ya wazi katika uwanja wa ndege wa N'dole, katika siku ya pili ya ziara ya papa barani Afrika.

Karibu nusu ya idadi ya watu wa Jamhuri ya demokrasia ya Congo ni wakatoliki -wakiwa ni jumuiya yenye wakatoliki wengi Zaidi barani Afrika. 

Akizungumza katika misa hiyo, kiongozi huyo wa wakatoliki ametoa wito wa amani nchini DR Congo, akisema upande unaopigana unapaswa kusameheana na kuwapa wapinzani wao "msamaha mkubwa kutoka moyo".

Aliendelea kusisitiza faida za kuondoa moyo wa "hasira na majuto, na kila dalili ya chuki na hasira".

Image: AFP

Kwaya ya watu 700, ambayo ilikuwa ikifanya mazoezi kwa pamoja kwa muda mrefu kwa ajili ya tukio hilo ambapo awali papa alitegemewa kufanya ziara mnamo Julai mwaka jana.

Ziara ya awali ya Papa ilibidi iahirishwe kwa sababu ya afya mbaya. 

Kumekuwa na manung'uniko kwamba Papa hajakosoa uongozi wa kisiasa wa DR Congo kama wengine walivyotarajia, lakini Misa ilikuwa tukio la furaha na papa alikuwa na ujumbe mzito wa amani kwa wale wanaohusika katika migogoro nchini humo. 

Mattieu Nzuzi, mmoja wa watu waliokuwa katika umati huo alisema anatumaini ziara ya papa itamaliza ghasia mashariki mwa nchi hiyo, karibu na mpaka na Rwanda: "Ninatumai kwamba ziara ya Papa nchini DRC italeta amani kwa nchi yetu kwa sababu huko karibu na Rwanda, watu wanateseka," alisema. 

Hata hivyo, siku ya pili ya ziara yake inaenda sambamba na mwendelezo wa mapigano kati ya jeshi la Kongo na waasi.

Misa ya Jumatano ilitajwa kuwa mojawapo ya misa kubwa zaidi kuwahi kutokea ya papa, ya pili baada ya ile iliyofanyika Ufilipino mwaka wa 2014, kulingana na Christopher Lamb, mwandishi wa Roma wa jarida la Kikatoliki The Tablet.

Katika mahojiano na kipindi cha redio cha BBC Newsday, alisema Ukatoliki unakua barani Afrika:

"Huu ndio mustakabali wa kanisa na ukuaji wa Kanisa Katoliki barani Afrika kwa kweli ni muhimu sana kwa mustakabali wa Ukatoliki."

Siku ya Jumanne, Papa alikutana na Rais Félix Tshisekedi na kutoa hotuba ya kulaani unyonyaji wa kihistoria wa rasilimali za Afrika, ambao aliutaja kama "ukoloni wa kiuchumi".

Pia alizungumzia changamoto ya DR Congo, kwa kuwa madini yamekuwa na jukumu muhimu katika vita kwa zaidi ya miongo mitatu:

"Mikono ya watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iachiliwe! Iacheni Afrika! Acheni kuiibia Afrika, sio mgodi au eneo la kuporwa."