Mwanasiasa, mke wahukumiwa kifungo baada ya kula njama ya biashara ya viungo vya binadamu

Obeta, alisema, aliwadanganya madaktari na kudai kuwa kijana huyo ambaye alitarajiwa kuwa mfadhili alikuwa binamu ya bintiye seneta

Muhtasari
  • Inasemekana kuwa kesi ya kwanza kama hii chini ya sheria za utumwa mamboleo.

Mwanasiasa tajiri wa Nigeria, mke wake na "mtu wao wa kati" wamefungwa kwa njama ya kusafirisha viungo vya binadamu, baada ya kuleta mwanaume mmoja nchini Uingereza kutoka Lagos.

Seneta Ike Ekweremadu, 60, na mkewe Beatrice, 56, walitaka kiungo hicho kwa ajili ya binti yao Sonia mwenye umri wa miaka 25, kesi ya wanandoa hao huko Old Bailey ilisikizwa.

Wawili hao na Dkt Obinna Obeta, 50, walipatikana na hatia hapo awali kwa kula njama ya kupata figo ya mwanaume huyo kwa ajili ya mtoto wao.

Inasemekana kuwa kesi ya kwanza kama hii chini ya sheria za utumwa mamboleo.

Ike Ekweremadu, alihukumiwa kifungo cha miaka tisa na miezi minane jela. Dkt Obeta alihukumiwa kifungo cha miaka 10 baada ya hakimu kupata kwamba alikuwa amemlenga mfadhili ambaye alikuwa kijana, maskini na asiye na uwezo.

Beatrice Ekweremadu alifungwa jela miaka minne na miezi sita kutokana na ushiriki wake.

Mwathiriwa, mfanyabiashara maskini wa mitaani huko Lagos, alipelekwa Uingereza kutoa figo kwa binti wa Ekweremadus.

Jaji Johnson alimtaja mwanasiasa huyo kama mtu wa ofisi ya juu mwenye mali nyingi, wafanyakazi wa ndani, vijakazi, wapishi na madereva ikilinganishwa na mwathiriwa, ambaye hakuweza kumudu tikiti ya pauni 25 ya kusafiri kwenda Abuja.

Obeta, alisema, aliwadanganya madaktari na kudai kuwa kijana huyo ambaye alitarajiwa kuwa mfadhili alikuwa binamu ya bintiye seneta ambaye alihitaji kupandikizwa kwa haraka.

Watatu hao walikuwa wamemwacha mfadhili anayetarajiwa kukabiliwa na "athari kubwa na ya muda mrefu katika maisha yake ya kila siku", alisema. "Usafirishaji haramu wa watu kuvuka mipaka ya kimataifa kwa ajili ya kuvuna viungo vya binadamu ni aina ya utumwa," jaji aliongeza.

Katika taarifa ya binafsi ya mwathiriwa, mfanyabiashara wa soko nchini Nigeria mwenye umri wa miaka 21, ambaye hawezi kutajwa kwa sababu za kisheria, aliiambia mahakama kwamba alikuwa akiomba kila siku ili apewe fursa ya kuingia Uingereza kufanya kazi au kusoma.