Meru: Mwanamke ahukumiwa Miaka 15 jela kwa kunyofoa nyeti za mumewe

Mama huyo alitumia kisu cha jikoni kutekeleza ukatili wake wakati mume alikuwa amelala.

Muhtasari

• Mama alimkata sehemu za siri kwa sababu ya mume wake kukataa kugawanya kipande chake cha shamba analolima miraa.

• Mwathiriwa anapokea matibabukwenye hopitali ya Chaaria Mission.

Mahakama
Mahakama
Image: MAHAKAMA

Mahakama ya Maua, Meru mnamo Novemba 23 2022 ilimhukumu mama wa watoto 5  kifungo cha miaka 15 jela baada ya kupatikana na hatia ya jaribio la kumuua mumewe kwa kumkata sehemu zake za siri kwa kisu.

Tukio hilo lilijiri siku ya Jumamosi ya Novemba 19 eneo la Igembe Kaunti ya Meru.

Kulingana na hukumu iliyotolewa na jaji mkuu Tito Gesora, mama huyo alinuwia kumuua mumewe alipokuwa amelala baada ya mume wake kukataa kugawanya shamba lake la miraa.

Mwanamume huyo alisimulia jinsi alivyoshtuka alipomwona mkewe akinyanyua kisu majira ya saa 3 asubuhi, akimpiga kichwa na kiungo chake cha siri huku akilia kwa maumivu. Mkononi alishika kisu cha jikoni alichotumia kutekeleza uhaini huo.

Mkulima wa miraa mwenye umri wa miaka 60, alijaribu kupiga kengele lakini alitokwa na damu nyingi hadi kupoteza fahamu.

Mahakama ilisema mkewe huyo katili hakutosheka, alijaribu kulazimisha kunywa kemikali isiyojulikana mdomoni mwa mumewe huku binti yao akijionea na akipiga kamsa baada ya mama mzazi kumuamuru anyamaze mara moja.

Mtoto alikimbia na kuomba msaada, na kuvutia wanakijiji ambao walikimbilia nyumbani wakiwa na hamaki kuu huku mama huyo akijaribu kuzua ghasia.

Mwanamke huyo kisha alijaribu kutoroka lakini wanakijiji walimkamata na kumpiga kitutu ila akaokolewa na chifu wa eneo hilo ambaye alimpeleka katika kituo cha polisi cha Laare.

Mume huyo sasa anaendelea kupata matibabu katika hospitali ya Chaaria Mission.

Mahakama ilipigwa na butwaa kumwona mkewe akimfanyia kitendo hicho licha ya kuoana kwa muda mrefu. Alisema alikataa kugawanya shamba lake kwa sababu  watoto wote walikuwa bado shuleni.

Mama aliiambia mahakama kuwa hakufahamu alichokuwa akifanya, alijikuta tu akimshambulia mumewe huku akijitetea kwamba hakukusudia na anaugua ugonjwa wa akili.