Mzee wa miaka 50 afungwa maisha kwa kumuoa msichana wa miaka 10

Saigulu alikiri kumnajisi msichana wa miaka kumi na kumuoa mwaka wa 2019.

Muhtasari

•Bi Shinyada alisema mwanamume huyo alionywa kuhusu ukubwa wa suala hilo baada ya kukiri mashtaka.

•Wakili wa serikali Tito Wanga alielezea kuridhishwa na uamuzi huo kufuatia uzito wa kosa hilo

Mzee Saigulu Ololosereka akiwa mahakamani leo wakati hukumu yake ikitolewa.
Image: ANN SALATON

Mahakama ya Narok imemhukumu mzee wa miaka hamsini kifungo cha maisha baada ya kukiri kosa la kunajisi na kumuoa msichana wa miaka kumi.

Saigulu Ololosereka ambaye alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Narok, Phyllis Shinyada alikabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni; kumnajisi msichana wa miaka kumi na kumuoa mwaka wa 2019.

Katika uamuzi wake, Bi Shinyada alisema mwanamume huyo alionywa kuhusu ukubwa wa suala hilo baada ya kukiri mashtaka lakini akashikilia kuwa alimuoa msichana huyo kwa sababu alitolewa kwake na wazazi wake.

“Kosa lililofanywa ni kubwa na la kinyama. Miaka mitatu iliyopita lazima ilikuwa miaka ya kutisha zaidi kwa mwathiriwa,” alisema hakimu.

Hakimu Mwandamizi aliendelea kusema kitendo hicho kiovu kilikuwa na athari ya kudumu ya kisaikolojia na kimwili kwani msichana huyo alifanyiwa ukeketaji kabla ya kuolewa na baadaye kufanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua.

Alibainisha kuwa mwanamume huyo hakuonyesha kujuta hata baada ya kuonywa juu ya ukubwa wa kosa hilo na badala yake alisisitiza kuwa msichana huyo ni mke wake ambaye wameoana naye kwa miaka mitatu.

"Aliomba tu msamaha na akajitetea kuwa hakumchukua msichana huyo kwa nguvu lakini wazazi walikuwa wamemkabidhi kwa ndoa, kumaanisha kwamba anahisi ana haki ya kuwa na msichana kama mke wake," alisema Hakimu Mwandamizi katika uamuzi wake.

Ukweli kwamba makosa kama hayo ni ya kawaida nchini ambapo wasichana hubadilishwa kwa mifugo au vitu vingine vya bei nafuu, Bi Shinyada alisema, inatoa adhabu kali ambayo itakuwa onyo kwa wengine wenye nia sawa.

Akimhukumu mzee huyo kifungo cha maisha jela, hakimu alisisitiza kuwa alizingatia umri wa msichana huyo ambaye alinajisiwa kiasi cha kupachikwa mimba na kwamba mwanaume huyo amekuwa akimnajisi mtoto huyo kwa miaka mitatu iliyopita.

Alimhukumu Ololosereka kifungo cha maisha jela kwa kosa la kwanza la unajisi, na miaka mitatu kwa shtaka la pili la ndoa ya mapema ambalo atalitumikia kwa wakati mmoja.

Wakili wa serikali Tito Wanga alielezea kuridhishwa na uamuzi huo kufuatia uzito wa kosa hilo.

Hata hivyo, mhalifu huyo alikumbushwa haki yake ya kukata rufaa katika mahakama ya juu zaidi katika muda wa siku 14 ikiwa hakuridhika na hukumu hiyo.