Wakili ampeleka fundi cherehani kortini kwa kuchoma suti yake wakati wa kuipiga pasi

Wakili huyo wa Nairobi alidai kwamba fundi cherehani alichoma suti yake ya Kiitaliano yenye thamani ya 35K wakati anajaribu kuichakachua kwa kuipiga pasi.

Muhtasari

• Mara ya kwanza, wakili huyo aliandikisha kesi hiyo katika mahakama inayoshughulikia madai madogo madogo.

• Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali kesi ya wakili huyo, jambo lililomfanya wakili huyo kuelekea mahakama ya juu akitafuta haki.

Pasi
Pasi
Image: HISANI

Wakili mmoja jijini Nairobi amemburuta fundi cherehani mahakamani kwa kile anadai kwamba fundi huyo aliichoma suti yake ghali ya Kiitaliano wakati anaipiga pasi.

Kwa mujibu wa ripoti kwenye The Standard, wakili huyo alidai fundi cherehani aliichoma suti yake ghali na kukubali makosa ambapo aliridhia kumlipa shilingi elfu 35.

Mara ya kwanza, wakili huyo aliandikisha kesi hiyo katika mahakama inayoshughulikia madai madogo madogo akisema kwamba fundi cherehani alikubali kumlipa shilingi elfu 3 kila mwezi hadi pale atakapokamilisha malipo ya elfu 35 lakini alifika katikati akagoma kufanya malipo.

“Katika kesi hiyo, Wakili G alisimulia kwamba alipeleka suti yake ya kijivu kwa fundi cherehani wakati fulani Mei 2021 kwa ushonaji nguo. Wakili huyo alieleza kuwa fundi cherehani aliomba radhi na kuahidi kumnunulia mpya na atamlipa Sh3,000 kuanzia wiki ya kwanza ya Julai mwaka huo,” ripoti hiyo ilisoma.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali kesi ya wakili huyo, jambo lililomfanya wakili huyo kuelekea mahakama ya juu akitafuta haki.

Mahakama ya juu katika uamuzi wa jaji Janet Mulwa, aliamua kwamba mahakama ya chini ilishindwa kubaini kwamba fundi cherehani alikuwa na makosa ya kuiharibu suti ghali kwani alifaa kuipeleka kwa dhobi wa kitaaluma ili kuifua na kuipiga pasi.

“Hakimu huyo msomi alikosea kisheria na kwa kweli kwa kushindwa kusisitiza kwamba uharibifu uliotokea kwenye suti la mdai ulitokana na uchakachuaji wa nguo na huo ulikuwa uthibitisho wa uzembe wa mlalamikiwa na mlalamikiwa kwa vile alikuwa fundi cherehani, taaluma isiyoruhusiwa na mila na desturi kupiga pasi nguo za ubora fulani ambazo zinafaa kupelekwa kwenye eneo la kufulia linalofaa kwa kufua au kunyoosha,” alihoji wakili mlalamishi.

Kesi hiyo yenye utata hata hivyo haikuweza kuamuliwa mara moja na itaendelea tena wiki hii.