Mahakama yatupilia mbali kesi dhidi ya Babu Owino

Babu na wengine sita waachiliwa huru

Muhtasari

•Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kutuma maombi ya kutaka kesi hiyo iondolewe mara moja

•Alikamatwa wakati wa maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali yaliyoidhinishwa na muungano wa Azimio la Umoja.

BABU OWINO.
Mbunge wa Embakasi Babu Owino BABU OWINO.
Image: FACEBOOK//BABU OWINO

Mahakama ya Nairobi imeondoa kesi ya jinai dhidi ya Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na washtakiwa wengine sita waliokuwa wanakabiliwa na mzozo huu.

Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kutuma maombi ya kutaka kesi hiyo iondolewe mara moja, kutokana na uamuzi wa mahakama kuu ambao ulitangaza shtaka la kupindua sheria kuwa kinyume na katiba.

“Nimezingatia mawasilisho pamoja na maombi yaliyotolewa na upande wa mashtaka ambayo bado yanatafakariwa na hivyo basi kesi hiyo imesitishwa,” alisema Hakimu Onyina.. Babu alikamatwa wakati wa maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali yaliyoidhinishwa na muungano wa Azimio la Umoja.

Alishtakiwa pamoja na Calvina Okoth Otieno almaarufu Gaucho, Tom Ondongo Ong'udi, Michael Otieno Omondi, Pascal Ouma, Kevin Wambo na Willys Owino Baraka.

Babu Owino sasa anasema atawasilisha kesi katika mahakama kuu ili kulipwa fidia kwani haki zao zilikiukwa wakati huo.

"Tutawasilisha ombi la kikatiba, tutatafuta fidia na gharama kutoka kwa serikali. Hatukutendewa haki, bila maji pamoja na chakula na  kunimwa huduma za mawakili wa kisheria," alisema Babu Owino.

Wakihutubia wanahabari baada ya uamuzi wa mahakama, mawakili wake Danstan Omari na Duncan Okatch walisema kwamba kuna uhuru wa kujieleza na kujumuika na ni wajibu wa serikali kuheshimu kifungu cha 37 cha katiba kuu ya Kenya.