Babu Owino ampa rais Ruto suluhu kumaliza mgomo wa madaktari, “Uza saa uwalipe!”

Owino alishauri rais Ruto kupiga mnada moja ya saa zake ghali za mkononi ili kupata fedha za kuwalipa madaktari ili warejee kazini. Hii ni baada ya rais Ruto kudai serikali haina pesa za kutosha kukidhi matakwa ya madaktari.

Muhtasari

• Pia aliwasisitizia madaktari kutokubali kufutilia mbali  mgomo wao hadi pale matakwa yao yatakaposikilizwa na kutekelezwa na serikali.

Rais Ruto na Babu Owino
Rais Ruto na Babu Owino
Image: FACEBOOK

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino amejibu kauli ya rais Ruto kwa madaktari kwamba hakuna pesa za kutosha kwenye hazina ya serikali kukidhi matakwa yao kwenye mgomo ikiwemo nyongeza ya mishahara.

Katika video moja ambayo mbunge huyo wa ODM alichapisha kwenye kurasa zake mitandaoni, alisema kwamba ana suluhu kwa rais Ruto kumaliza mgomo wa madaktari ambao upo katika wiki ya tatu sasa na kulemaza shughuli nyingi za matibabu kwenye hospitali za umma humu nchini.

Owino alishauri rais Ruto kupiga mnada moja ya saa zake ghali za mkononi ili kupata fedha za kuwalipa madaktari ili warejee kazini.

“Jana nilisikia Ruto akiongea kwamba hana pesa ya kuwalipa madaktari. Huwezi kutuambia kama rais kwamba hakuna pesa hali ya kuwa saa unayovaa ni ya bei ghali. Uza hiyo saa na ulipe madaktari,” Owino alisema.

Pia aliwasisitizia madaktari kutokubali kufutilia mbali  mgomo wao hadi pale matakwa yao yatakaposikilizwa na kutekelezwa na serikali.

“Tunaambia madaktari kesho mumeweka maandamano, hayo maandamano yaendelee.”

Mbunge huyo alikwenda mbele na kunukuu kifungu cha Biblia kuhusu baba kuwaachia wanawe urithi wa maana.

“Biblia inasema kwamba kama mwanao atakuomba mkate, unafaa kumpa jiwe? Na kama anakuomba samaki unampa nyoka? Kwa hivyo watoto wako ambao ni madaktari wameuliza, wapatie samaki, na wapatie mkate. Hii Kenya kuna pesa, ushuru uliongeza, na kuna pesa nyingi,” Owino alimshauri rais.

Mgomo wa madaktari umeendelea kwa karibia mwezi sasa wakitaka mkataba wa CBA wa 2017 kutekelezwa ikiwemo kuongeza madaktari wanagenzi malipo kutoka elfu 70 hadi 204k.

Wikendi, katibu mkuu wa muungano wa madaktari KMPDU, Devji Atellah alisema shughuli za matibabu zitaendelea kutatizika kote nchini na hata kuitisha maandamano mengine Jumanne hii leo.