Mombasa: Mrembo wa miaka 23 achomwa kwa mafuta moto usoni na mpenzi wake

"Hakuna daktari aliyekuja kumsaidia, na wale wanakuja wanamuangalia na kunipa kazi ya kumuosha kumfanya kila kitu na sijui vile mgonjwa wa kuchomeka anaoshwa,” mamake alilia.

Muhtasari

• Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kusikitisha katika runinga ya NTV, Isaac Ayinga, kijana anayeshukiwa kumtendea Wangeci unyama huo bado yuko mafichoni.

Maji moto
Maji moto
Image: BBC

Mrembo mwenye umri wa miaka 23 kaunti ya Mombasa analilia haki baada ya kudai kuchomwa usoni kwa mafuta moto na mpenzi wake.

Deborah Wangeci, sasa anapitia wakati mgumu kufuatia mgomo wa madaktari katika hospitali za umma ambao umegonga wiki mbili sasa.

“Ameniharibia sura, sijui nitaanzia wapi, hata nikitoka hapa sijui kama nitakula,” Wangeci alisema akiwa katika maumivu makali kitandani hospitalini.

Kwa mujibu wa mama yake, binti yake anazidi kuungulia maumivu ya kuchomeka usoni huku madaktari wakiwa si wa msaada kwake na sasa imemlazimu kumhamishia katika hospitali ya kibinafsi licha ya gharama kuwa kubwa.

“Mtoto wangu sasa hakuna kazi anaweza fanya mikono imeumia. Mwili wote umeumia mpaka kwa maziwa. Alikuwa na maumivu mengi sana ya mwili, na analia madaktari wamsaidie, hakuna daktari aliyekuja kumsaidia, na wale wanakuja wanamuangalia na kunipa kazi ya kumuosha kumfanya kila kitu na sijui vile mgonjwa wa kuchomeka anaoshwa,” mamake alilia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kusikitisha katika runinga ya NTV, Isaac Ayinga, kijana anayeshukiwa kumtendea Wangeci unyama huo bado yuko mafichoni.

Galib Salim, katibu wa muungano wa madaktari tawi la Mombasa alisema kwamba wanaonea wagonjwa huruma lakini ni wakati pia hata wananchi wenyewe wasimame kidete na kushinikiza serikali kukidhi matakwa yao ili kurejea kazini.